Daftari la kudumu la Wapiga Kura! Kumekucha, semeni mengine!
Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amezindua zoezi la uboreshaji wa daftari la
kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR) na kuwataka
viongozi wa siasa wawahimize wanachama wao wajitokeze kwa wingi bila kujali tofauti
za kiitikadi. Ametoa wito huo Jumanne, Februari 24, 2015 wakati akizungumza na viongozi
mbalimbali na wananchi waliofika kushuhudia uzinduzi huo uliofanyika kwenye kata ya
Lumumba, Halmashauri ya Mji wa Makambako, mkoani Njombe. “Ninawasihi viongozi wa
siasa tuwahimize wanachama wetu waende kujiandikisha kwa wingi. Tuache kauli za kukatisha
tamaa, tuache kauli za kejeli sababu zoezi hili ni jema na lina nia ya kuwawezesha
Watanzania wote kutumia haki yao ya kupiga kura,”alisema. Waziri Mkuu alitumia fursa
hiyo kuwaomba Watanzania wenye vitambulisho vya uchaguzi vya zamani na wale wasio
na vitambulisho wajitokeze kwa wingi kushiriki zoezi hilo. “Wale waliokwishafikisha
miaka 18, na wale ambao watatimiza miaka 18 ifikapo Oktoba, mwaka huu wajitokeze kwa
wingi kujiandikisha kwa sababu wasipofanya hivyo hawataweza kupiga kura kama hawatajiandikisha
kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” aliongeza. Akiwa uwanjani hapo, Waziri
Mkuu alishuhudia uandikishaji wa wakazi watatu wa kata hiyo ambapo zoezi zima lilidumu
kati ya dakika tatu na dakika tano. Kisha alikabidhi kadi kwa mpigakura wa kwanza
kuandikishwa ambaye alitumia dakika tatu kamili. Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema amefurahishwa na taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva kwamba zoezi la uandikishaji lililoanza jana katika mji
wa Makambako lilizidi matarajio ya Tume ya kuandikisha wapigakura 1,850. “Nimefarijika
sana na taarifa ya Mwenyekiti... Mlianza na kata tisa zenye vituo 54 na mlitarajia
kuandikisha watu 1,850 lakini badala yake mmepata watu 3,014. Hili limenipa faraja
sana. Ninawapongeza sana kwa hatua hiyo,” alisema. Mapema, akitoa taarifa kabla
ya kumkaribisha Waziri Mkuu kufanya uzinduzi huo, Jaji Lubuva alisema ana imani wadau
mbalimbali wataendelea kuhamasisha wananchi washiriki zoezi la uboreshaji daftari
la wapiga kura. Alisema uboreshaji wa daftari hilo utafanyika kikanda na kwamba
wamepanga kutumia siku saba kwa kila kituo huku akisisitiza kwamba hakuna mtu atakayebakizwa
bila kuandikishwa wakati ameshafika kituoni. Aliwataka watu wanaokwenda kujiandikisha
wawe na vitambulisho vyao vya zamani vilivyotolewa na Tume ya taifa ya Uchaguzi kwani
tayari vina taarifa zao kwa hiyo vitapunguza muda wa mtu kuandikishwa. “Kadi za Tume
(NEC) au za NIDA kwa wale wachache ambao wanazo, wakija nazo zitapunguza muda wa uandikishai
sababu zina taarifa kwenye kanzidata,” alisema. Akitoa ufafanuzi kuhusu mfumo wa
uandikishaji wa BVR, Jaji Lubuva alisema mfumo huo siyo sawa na mfumo wa upigaji kura
wa kielektroniki (e-voting) kama ambavyo wengi wanadai bali mfumo huo unafanya kazi
kwa kutumia alama muhimu za mpigakura. “Mfumo huu unatumia alama zaidi kwanza ikiwa
ni picha na zaidi ni macho ya mhusika, pili ni alama za vidole na tatu ni saini ya
mhusika. Mfumo huu unaweza pia kuchukua alama za mtu mwenye ulemavu wa kuona ama ulemavu
wa mikono,” alisema. Alisema uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ni hatua
ya kisheria na kwamba Tume itajitahidi kuhakikisha inafuata hatua zote wakati wa zoezi
hilo. Waziri Mkuu ameondoka Makambako na anaelekea Mbeya kuanza ziara ya kikazi
ya siku sita kukagua shughuli za maendeleo katika mkoa huo.