Kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakayofanyika
mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015, Baraza la Maaskofu Katoliki
Afrika ya Kusini limetuma maswali dodoso 42 kwenye mitandao ya kijamii ili kuwashirikisha
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoa maoni, mawazo na tafakari kuhusu masuala
kadhaa kuhusu maisha ya ndoa na familia, ili hatimaye, kuyafanyia kazi, tayari kuyawasilisha
kwenye Sekretarieti kuu ya Sinodi mjini Vatican, tayari kwa ajili ya maandalizi ya
hati ya kutendea haki, yaani “Instrumentum Laboris”. Maswali haya
dodoso yamechukuliwa kutoka kwenye Hati ya Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu iliyofanyika
mwezi Oktoba, 2014. Itakumbukwa kwamba, kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Sinodi
ya maaskofu kuhusu familia ni “Wito na utume wa familia katika Kanisa na Ulimwengu
mamboleo”. Maoni na mchango wa waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Afrika ya
Kusini, utawasaidia Maaskofu kuwa na mawazo mapana zaidi kuhusiana na halisi ya maisha
na utume wa watu wa ndoa na familia. Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini
linapania kupata walau mwanga wa matatizo maalum yanayogusa maisha na utume wa familia
nchini humo. Kutokana na sababu mbali mbali wanasema Maaskofu kuna familia ambazo
kwa sasa zinaendeshwa na watoto wadogo. Waamini wanaweza kuwasilisha maoni yao hadi
tarehe 27 Machi, siku chache kabla ya Maaskofu hawajawasilisha mawazo yao kwenye Sekretarieti
kuu ya Sinodi ya Maaskofu hapo tarehe 15 Aprili 2015. Taarifa zinaonesha kwamba,
Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia zimeamua kutuma maswali dodoso kwa waamini
na watu wenye mapenzi mema kwa njia ya mitandao ya kijamii, ili kupata mawazo ya wengi,
licha ya utaratibu unaotumiwa na Kanisa katika kupata taarifa zake. Lakini itakumbukwa
kwamba, kwa mara ya kwanza hata Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu ilichapisha
maswali dodoso kwenye mtandao ili kuwapatia watu wengi zaidi kushiriki na matokeo
yake yalikuwa kweli ni ya kushangaza. Kumbe si bure, kuona watu wengi wanafuatia
kwa kina na mapana maadhimisho ya Sinodi kwa ajili ya familia, kwani hapa ni kitovu
cha maisha na matumaini ya binadamu kwa sasa na kwa siku za usoni. Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.