Serikali nchini Angola kushirikiana na Makanisa katika sekta ya elimu!
Baraza la Makanisa nchini Angola, CICA linaendelea kuimarisha mshikamano wa umoja
na udugu kati ya Makanisa pamoja na Serikali katika sekta ya elimu na majundo makini
kwa vijana wa kizazi kipya. Hizi ni juhudi zilizofanikishwa kati ya Bwana Manuel Vicente,
Makamu wa Rais nchini Angola alipokutana na kuzungumza na viongozi wa Makanisa nchini
humo. Makamu wa Rais amekazia umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na Makanisa,
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya vijana wa kizazi kipya nchini Angola, ili kuwajengea
imani na matumaini mapya yatakayosaidia kukoleza mchakato wa maendeleo yao kiroho
na kimwili, kwa kujikita pia katika utu wema na kanuni maadili, dhamana ambayo inaweza
kutekelezwa barabara na viongozi wa kidini. Mama Deodolinda Dorcas Tecas, Katibu
mkuu wa Baraza la Makanisa nchini Angola amesema, Serikali inataka kuhakikisha kwamba,
inaunganisha nguvu kwa kushirikiana na Makanisa katika mchakato wa maboresho ya elimu
nchini humo. Lengo ni kusaidia kutoa elimu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu
na hatarishi; vijana wanaotumia dawa haramu za kulevya pamoja na kuendelea kuogelea
katika ulevi wa kupindukia, jambo linalochangia ajali nyingi barabarani, ujambazi
pamoja na uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu nchini Angola. Baraza la
Makanisa Angola kwa kushirikiana na Serikali litawekeza zaidi katika huduma kwa makundi
haya ya vijana, ili kuyasaidia kugundua tena ndani mwao, kwamba, wameumbwa kwa sura
na mfano wa Mungu, wanapendwa na kuthaminiwa na Kanisa na Jamii katika ujumla wao,
kumbe ni wajibu wao kuenenda katika utu wema, kwa kuheshimu maisha, ambayo ni zawadi
kubwa kutoka kwa Mungu. Makanisa yatafanya kazi bega kwa bega na Wizara ya elimu,
familia, maendeleo ya wanawake pamoja na wizara ya utamaduni. Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.