Chansellor Angela Merkel baada ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko
mjini Vatican, mwishoni mwa juma, alikwenda kutembelea Jumuiya ya Mtakatifu Egidio
yenye makao makuu yake mjini Roma na kupokelewa na viongozi wakuu wa Jumuiya hii ambayo
imekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa jamii. Chansellor Angela Merkel amezungumza kwa kina na mapana na viongozi
hawa kuhusu mikakati ya amani na maridhiano kati ya watu wa mataifa; tatizo na changamoto
kwa wahamiaji wanaoendelea kuwasili kwa wingi Barani Ulaya kupitia bahari ya Mediterrania
ambako wengi wao wanazidi kupoteza maisha au kutumbukizwa katika biashara haramu ya
binadamu. Viongozi hawa wamegusia pia hali ya Bara la Ulaya na changamoto zake zinazogumisha
mshikamano na mfungamano wa kijamii kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Kwa
upande wake, Bwana Marco Impagliazzo, Rais wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, katika
hotuba yake ya kumkaribisha Angela Merkel, amegusia mafanikio ya upatikanaji wa amani
huko Msumbiji, Guatemala na Burundi. Wanampongeza kwa juhudi zinazofanywa na Serikali
ya Ujerumani ii kusitisha vita na kuanza mchakato wa ujenzi wa amani nchini Ukraine,
ili watu waanze tena kujikita katika maendeleo na ustawi wao baada ya vita. Juhudi
za kujenga na kudumisha amani ni kati ya vipaumbele vya kwanza vinavyofanyiwa kazi
na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio sehemu mbali mbali za dunia kwani wanatambua kwamba,
vita na kinzani ni mama wa umaskini. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inatambua na kuthamini
juhudi za kidiplomasia katika kutatua migogoro na kinzani mbali mbali kwani juhudi
hizi ni mwanga na matunda ya kitamaduni na kiutu yanayojikita katika imani na kwamba,
matokeo yake ni amani ya kudumu. Jumuiya hii imekuwa ikijielekeza zaidi katika majadiliano
ya kidini na kiekumene; kisiasa na kitamaduni kwamba, amani inachangia kwa kiasi kikubwa
ustawi na maendeleo ya watu. Dini mbali mbali duniani zina dhamana ya kuendeleza
mchakato wa amani na maridhiano kati ya watu; kwa kukuza na kudumsiha tunu msingi
za maisha ya kiroho na kiutu, ili kweli amani iweze kuzama katika maisha na vipaumbele
vya watu, changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo. Wananchi wengi wa Bara la Ulaya
wanaogopa kukutana na kuchangamana na watu kutoka katika Mabara mengine, Jumuiya ya
Mtakatifu Egidio, inawasaidia kuvuka mwono huu finyu. Jumuiya hii inajikita katika
mambo makuu matatu: sala, maskini na amani na inatekeleza dhamana na utume wake katika
nchi 73 duniani. Inapania kumwilisha Injili ya Furaha, Amani, Ukarimu na Matumaini
kwa wale waliokata tamaa pamoja na kukosa uhuru ambao kimsingi ni haki yao sanjari
na kukumbatia mafao na furaha ya wengi. Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.