Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana limechapisha muhtasari wa mbinu muhimu za kufundishia,
ili kuhakikisha kuwa, wananchi wa Ghana wanapata elimu bora zaidi itakayowasaidia
kupambana na mazingira, ili yaweze kuwa bora zaidi. Kanisa linapenda kuhakikisha kwamba,
wanafunzi wanapohitimu masomo yao, wawe wamepikwa na kuiva barabara tayari kuchangia
katika ustawi na maendeleo yao binafsi, familia, jamii na taifa katika ujumla wake.
Hii ni elimu inayomwandaa mwanafunzi kwa ajili ya uwajibikaji na maisha kwa siku
za usoni. Muhtasari huu umezinduliwa hivi karibuni na Askofu Mathew Gyamfi, Mwenyekiti
wa Tume ya Elimu, Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana, ambaye anakazia kwamba, kuna
haja ya Serikali, Kanisa na wadau mbali mbali wa elimu kushirikiana kwa karibu zaidi,
ili kuhakikisha kwamba, elimu inayotolewa inazingatia viwango, taaluma na kumhusisha
mtu mzima, dhamana inayopaswa sasa kutekelezwa na wadau mbali mbali katika shule,
taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu nchini Ghana. Kanisa limeamua kuivalia njuga
sekta ya elimu baada ya kuona kwamba, elimu nchini Ghana ilikuwa inachechemea kiasi
cha kukatisha tamaa na kwamba, watu walianza kukata tamaa ya kuendelea na masomo,
kwani elimu ilionekana kutokuwa na msaada mkubwa kwa wananchi wengi licha ya jitihada
zilizokuwa zinafanywa na wadau mbali mbali. Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana
linapenda kujielekeza zaidi katika huduma ya elimu kwa wanawake ili kuweza kuwaletea
ukombozi wa kweli, ili hatimaye, waweze kuchangia katika ustawi na maendeleo ya familia
na jamii kwa ujumla wake. Maaskofu wanabainisha mambo msingi ambayo yanapaswa kutekelezwa
na walimu kwa kukazia nidhamu, weledi, juhudi, bidii na maarifa yatakayowawezesha
kurithisha elimu kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuwajengea uwezo wa kupenda
kusoma na kujiendeleza zaidi kwa kutambua kwamba, elimu ni mkombozi wa maisha ya mwanadamu. Muhtasari
huu anasema Askofu Mathew Gyamfi unapembua mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu
nchini Ghana; mafanikio, matatizo, changamoto na jinsi ambavyo Kanisa limefanikiwa
kufanya maboresho makubwa katika sekta ya elimu katika shule, taasisi na vyuo vinavyomilikiwa
na Kanisa, kwa ajili ya mafao ya wengi. Haya ndiyo mang’amuzi ambayo Kanisa linapenda
kuishirikisha Serikali, ili kukoleza mchakato wa mageuzi ya kina nchini Ghana, katika
medani mbali mbali za maisha. Kanisa Katoliki ni mdau mkubwa katika sekta ya elimu,
utume ambao umefanywa kwa majitoleo makubwa tangu Wamissionari walipoingia Barani
Afrika. Kanisa nchini Ghana linamiliki na kuendesha taasisi 4, 000 za elimu kuanzia
elimu ya awali hadi chuo kikuu. Kanisa litaendelea kujielekeza katika maboresho ya
sekta ya elimu ili kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini ya maisha bora kwa
njia ya elimu makini, kwa kushirikiana na wadau mbali mbali. Huu ni mradi mkubwa ambao
Kanisa limeishirikisha Serikali ya Ghana, ili kushirikiana kwa pamoja katika ustawi,
maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Ghana. Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.