2015-02-23 09:14:47

Linda moyo wako!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, aliwagawia waamini na mahujaji waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, nakala 50, 000 za kitabu kinachobebeka mfukoni, “Linda moyo wako”. Hizi ni juhudi za Baba Mtakatifu zinazolenga kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukiishi vyema Kipindi cha Kwaresima, muda muafaka wa toba na wongofu wa ndani, unaomwilishwa katika matendo ya huruma.

Kati ya wadau waliokuwa wanagawa vitabu hivi ni watu 100 wasiokuwa na makazi maalum, watu ambao kwa sasa wanapewa upendeleo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kuboresha maisha yao, kwani hawa ni hazina kubwa ya maisha na utume wa Kanisa; ni watu ambao wameonja Injili ya Furaha na kwa sasa wako tayari kutoka kifua mbele kutangaza matendo makuu ya Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni Wakristo shupavu katika maisha na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; ushupavu unaopata chimbuko lake katika undani wa moyo wa mtu. Kitabu hiki chenye kurasa thelathini, kinabaisha kwa kina na mapana mambo msingi ambayo yanaweza kumsaidia mwamini kuwa kweli ni shupavu wa imani, kwa kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuufunda moyo, ili uweze kufanana na Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mchungaji mwema, aliyethubutu kujisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwaresima ni kipindi kinachotoa mwaliko kwa waamini kutubu na kumwongokea Mungu, kwa kuanzia kutoka katika undani wa mioyo yao; uwanja unaotumika kwa ajili ya kufanya maamuzi mema au mabaya; kwa kukumbatia Injili au kumezwa na malimwengu; kwa kujikita katika uchoyo na wivu au kwa kushirikishana na kumegeana na wengine, kile ambacho Mwenyezi Mungu amekujalia katika maisha.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2015 anawasihi waamini kumwomba Kristo awasaidie kuunda mioyo yao, ili iweze kufanana na Moyo wake Mtakatifu tayari kuweza kuwa na nguvu, makini na wenye huruma kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani sehemu mbali mbali za dunia, ili kujenga na kuimarisha utandawazi wa upendo, udugu na mshikamano wa kweli.

Kitabu hiki kinatoa kwa muhtasari mafundisho makuu ya Yesu kwa wanafunzi wake: kuhusu heri za mlimani, mwaliko wa kuwa watakatifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo Mtakatifu, wajitahidi kujiwekea akiba mbinguni, wasamehe na kusahau; wasihukumu bali wajikite katika kanuni ya dhahabu pamoja na kujitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na kwa njia ya ushuhuda huu wa maisha, kwa hakika wataweza kutambulikana kuwa kweli ni wafuasi wa Yesu Kristo.

Kitabu hiki kinafafanua Kanuni na mafumbo makuu ya imani; fadhila kuu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo; Sakramenti za Kanisa na matunda kumi na mawili ya Roho Mtakatifu; Amri za Mungu na za Kanisa; matendo ya huruma ya kiroho na kimwili; fadhila kuu nne na vilema saba vya dhambi. Kimsingi huu ni muhtasari wa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujisomea na kulitafakari Neno la Mungu, ili waweze kulimwilisha katika matendo na vipaumbele vya maisha yao; wajijengee utamaduni wa kuchunguza dhamiri kila siku jioni kadiri ya Mapokeo ya Kanisa. Anawaalika waamini kutunza hazina ya mioyo yao na kamwe wasiugeuze mioyo yao kuwa ni uwanja wa fujo, bali mahali patakatifu ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza na mja wake. Waamini wanaalikwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Baba Mtakatifu anafafanua kwa kina na mapana kwanini waamini wanaalikwa kuungama dhambi zao; anawaelekeza namna bora ya kuungama ili kupata msamaha wa dhambi, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu mioyoni mwao; ni mambo yepi ya kuungama mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kutotimiza wajibu kwa Mungu, jirani na katika maisha ya mtu binafsi. Baba Mtakatifu anawasaidia waamini kuchunguza vyema dhamiri zao na hatimaye kusali ile sala ya kutubu.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, kuwa na moyo wenye huruma na mapendo ni kujiweka wazi mbele ya Mungu, ili kumruhusu Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi yake kwa kumwelekeza mwamini kuwaonjesha jirani zake upendo. Huu ni moyo unaotambua mapungufu yake, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.