2015-02-23 08:52:51

Licha ya mtutu wa bunduki DRC, Kanisa linaendelea kuwekeza katika elimu!


Kanisa Katoliki nchini DRC licha ya magumu na changamoto nyingi zilizopo nchini humo, bado linaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kukazia majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya. Hivi karibuni, Askofu Nicolas Djomo Lola, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC alizundua Kituo kipya cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki Kinshasa, kinachotarajiwa kuanza kufanya kazi hapo tarehe 27 Februari 2015.
Askofu Nicolas Djomo Lola amezindua kituo hiki katika Ibada ya Misa takatifu iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu nchini DRC. Lengo la Kanisa ni kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina Barani Afrika, unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kama wanavyokazia Mababa wa Sinodi ya Afrika. Chuo kikuu cha Kikatoliki ni mahali ambapo, wanafunzi wanajifunza tunu msingi za maisha ya Kiinjili, kiutu na kitamaduni, tayari kujisadaka katika huduma kwa ndugu zao.
Serikali ya DRC inalipongeza Kanisa kwa kuendelea kuwa ni mdau mkubwa katika sekta ya elimu. Kanisa linaiomba Serikali kulisaidia kuchangia gharama za uendeshaji kwa ajili ya mafao ya wananchi wake, kwani hadi sasa Kanisa limekuwa likiendesha: shule, taasisi za elimu na vyuo vikuu nchini humo kwa ufadhili kutoka ndani na nje ya nchi.
Ujenzi wa Kituo kipya cha Chuo kikuu cha Kikatoliki Kinshasa ulianza kunako mwaka 2009. Hapa kuna vitivo vya: Taalimungu, Sheria za Kanisa, Falsafa, Uchumi na Maendeleo, Mawasiliano ya Jamii, Sheria na Sayansi Jamii. Kuna jumla ya wanafunzi 2, 000.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.