Familia ya Mungu nchini Tanzania, mwishoni mwa Juma, ilikusanyika kwa ajili ya kumsindikiza
Marehemu Askofu mstaafu Magnus Mwalunyungu wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi aliyefariki
dunia hivi karibuni katika usingizi wa amani. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na
Askofu mkuu Damian Dallu wa Jimbo kuu la Songea, katika Parokia Tosamanga, Jimbo Katoliki
Iringa, aliyewataka waamini kutoogopa kukabiliana uso kwa uso na Fumbo la Kifo na
badala yake wajiandae kikamilifu kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele.
Katika
mahubiri yake Askofu mkuu Dallu anasema kwamba, Marehemu Askofu Mwalunyungu ameishi
kwa muda wa miaka 85 na kati ya hiyo, miaka 55 amelitumikia Kanisa kama Padre na miaka
mingine 13 kama Askofu. Baada ya kung'atuka kutoka madarakani aliendelea kumtumikia
Mungu kwa njia ya huduma Parokiani, akawa Paroko wa kwanza wa Parokia ya Kidamali,
Jimbo Katoliki la Iringa, utume ambao umeufanya kwa miaka minne. Hiki ni kifo cha
mwadilifu ambaye kwa sasa anapumzika kwa amani na starehe mbele ya Mwenyezi Mungu.
Ibada
hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na Familia ya Mungu nchini Tanzania. Waziri mkuu
wa Tanzania, Mizengo Pinda amemwakilisha Rais Jakaya Kikwete ambaye amewataka watanzania
kufuata mafundisho yanayotolewa na viongozi wao wa dini, ili kujenga moyo wa uchaji
wa Mungu, uadilifu na unyofu.