Amani na utulivu kamwe havitaweza kupatikana katika uso wa dunia, ikiwa kama baa la
njaa halitaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na Jumuiya ya Kimataifa. Kuna kundi la
watu wachache wanaokula na kusaza kiasi hata cha kutupa chakula na wakati huo huo
kuna bahari ya watu wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na baa la njaa na utapiamlo
wa kutisha duniani. Hii ni changamoto inayotolewa na Baraza la Kipapa la haki na amani
katika hati inayojulikana kama "Dunia na Chakula" iliyotiwa mkwaju na Kardinali Peter
Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani.
Baraza la
Kipapa la haki na amani linabainisha kwamba, kuna haja ya kufanya marekebisho makubwa
katika mfumo mzima wa uzalishaji, ugavi, matumizi ya rasilimali pamoja na mtindo wa
maisha. Kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, chakula ni haki msingi ya binadamu,
kwani ina mahusiano makubwa na maisha ya mwanadamu, kwani pasi na chakula, maisha
ya mwanadamu yako hatarini, ndiyo maana Waswahili wanasema, eti "Njaa ni mwanaharamu..."
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kukazia matumizi bora ya rasilimali ya dunia
kama kikolezo cha kupambana na baa la umaskini, linaloendelea kudhalilisha utu na
heshima ya binadamu; hali ambayo kimsingi inahitaji usawa na haki, ili kweli baa la
umaskini liweze kupewa kisogo.
Hati hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu:
Sehemu ya kwanza inasema hali inatisha. Baraza la Kipapa la haki na amani linafafanua
kwa kina na mapana mambo yanayoendelea kuchangia uwepo wa baa la njaa licha ya uzalishaji
mkubwa wa mazao ya chakula.
Sehemu ya pili ya Hati hii inazungumzia mchango
wa Kanisa katika kufanikisha mchakato wa maboresho katika sekta ya kilimo, kwa kuangalia
vifungu vya Maandiko Matakatifu pamoja na Mafundisho mbali mbali yaliyokwishawahi
kutolewa na Mababa wa Kanisa kuhusiana na mada hii. Baraza la Kipapa la haki na amani
linabaianisha kanuni msingi katika tafiti na sera zinazoweza kutumika katika kupambana
na baa la njaa duniani. Sehemu ya tatu inazama zaidi katika kutoa majibu muafaka kwa
changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo kwa kujikita katika mwelekeo wa kitamaduni
na sera ambazo, kama zikitumika kwa usahihi zinaweza kuwa ni "Mwarobaini" wa baa la
njaa duniani.
Takwimu zilizotolewa na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja
wa Mataifa, FAO zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2012 hadi mwaka 2014 kumekuwepo
na zaidi ya watu millioni 805 waliokuwa wanakabiliwa na baa la njaa na utapiamlo wa
kutisha, kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hili ni janga la kimataifa na wala hapa
hakuna utani kwani maisha ya watu wengi yako hatarini kutokana na baa la njaa.
Inasikitisha
kuona kwamba, dunia inaweza kuzalisha chakula cha kutosha kulisha watu wote duniani,
lakini kutokana na ubinafsi, uchoyo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko
ya wengine kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko, leo hii bado kuna watu wanafariki
dunia kwa kukosa chakula! Kumekuwepo na mahitaji ya chakula hasa kutoka katika Nchi
zinazoendelea duniani, lakini bado hakuna majibu yanayotosheleza mahitaji haya.
Hapa
kuna haja ya kuwa na mtazamo mpana zaidi wa kuchambua na kuangalia mambo, kwani kuna
mambo mengi yanayoendelea kuchangia uwepo wa baa la njaa duniani. Kwa mfano: vita
na kinzani za kijamii na kisiasa; ongezeko la bei ya mazao ya chakula; maafa asilia
kama vile ukame na mafuriko; rushwa na ufisadi. Bado Jumuiya ya Kimataifa haija fanikiwa
kutoa chakula cha kutosha kwa kila mwanadamu kutokana na kushindwa kufanya mageuzi
katika miundo ambayo imechangia uwepo wa baa la njaa duniani.
Matumizi mabaya
ya ardhi ni jambo ambalo linaendelea kusababisha ukosefu mkubwa a chakula duniani
na hata wakati mwingine, ardhi ambayo inafaa kwa kilimo cha mazao ya chakula, imegeuzwa
na sasa inatumika kwa ajili ya kuzalisha nishati uoto. Ukosefu wa mvua za kutosha
na maji kwa ajili ya kilimo cha umwagaliaji ni mambo ambayo pia yanachangia uwepo
wa baa la njaa mwaka hadi mwaka. Uchafuzi wa mazingira pamoja na athari za mabadiliko
ya tabianchi bado ni kikwazo kikubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Kumekuwepo na ukataji miti ovyo pamoja na mashirika ya biashara ya kimataifa
kuendelea kuneemeka kwa kupewa maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya kilimo cha kisasa,
lakini wakulima wadogo wadogo, wakiondolewa kutoka katika maeneo ambayo walikuwa wanayatumia
kwa ajili ya kuzalisha mazao ya chakula na biashara kwa ajili ya familia zao, huu
ni ukoloni mamboleo.
Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
XVI pamoja na Papa Francisko ni kati ya viongozi wa Kanisa ambao wamechangia kwa kiasi
kikubwa katika kuwahamasisha walimwengu umuhimu wa kujenga na kudumisha mshikamano
wa upendo kama sehemu ya mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; utandawazi
unaojikita katika ubinafsi, uchu wa mali na faida kubwa. Baadhi ya wafanyabiashara
wanaona mazao ya chakula kuwa kama bidhaa inayoweza kuwaingizia faida kubwa na kusahau
kwamba, chakula ni haki msingi ya binadamu.
Baraza la Kipapa la haki na amani
linabainisha kwamba, Mwenyezi Mungu baada ya kumuumba mwanadamu alimkabidhi ardhi
ili aweze kuitumia na kuiendeleza. Kumbe, rasilimali ardhi ni kwa ajili ya mafao ya
wengi; inayopaswa kutumiwa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, kwa kuzingatia
kanuni ya auni, haki, utu na heshima ya binadamu.
Sehemu ya tatu ya Hati ya
Baraza la Kipapa la haki na amani kuhusu Dunia na Chakula inabainisha sera na mikakati
inayoweza kutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa katika kuendeleza kilimo bora kinachozingatia
na kuheshimu maisha ya mwanadamu, ili kupambana kufa na kupona na baa la njaa ambalo
linaendelea kunyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Ekolojia na maendeleo
ni mambo yanayopaswa kuwa na mlinganyo mzuri, ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu
ya binadamu.
Baraza la Kipapa la haki na amani, linahamasisha uwekezaji bora
katika sekta ya kilimo, ili kupunguza athari za ukosefu wa usalama wa chakula katika
eneo husika sanjari na kuchangia ustawi na maendeleo ya watu. Haki msingi za binadamu
zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kuhakikisha kwamba, maisha yanalindwa na
kudumishwa; watu wanapata chakula bora na maji safi na salama; wanafundishwa mbinu
za kilimo bora na cha kisasa linachoheshimu na kutunza mazingira.
Wananchi
washirikishwe katika kupembua na kufanya maamuzi kuhusu hatima ya maisha yao; wapewe
mikopo na taasisi za elimu zijengewe uwezo wa kufanya tafiti na matokeo yake kuwasilishwa
kwa wahusika, ili yaweze kufanyiwa kazi. Hapa kuna haja ya kuachana na kasumba ya
kufanya tafiti na baadaye kuzifungia kwenye makabati ofisini.
Njia za mawasiliano
ya kibiashara hazina budi kuboreshwa; kudhibiti matumizi mabaya ya chakula na raslimali
ya dunia; kuwafunda na kuwaelimisha wawekezaji katika sekta ya kilimo; kuwasaidia
wafanyabiashara na wanasiasa kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara.
Baraza
la Kipapa la haki na amani linabainisha kwamba, Kanisa Katoliki linashiriki kikamilifu
ili kuhakikisha kwamba, watu binafsi, taasisi na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla
wake, zinajifunga kibwebwe ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula. Kanisa
linatekeleza dhamana hii kwa kutumia Mashirika yake ya misaada kimataifa na kitaifa,
Mabaraza ya Maaskofu Katoliki na miundo yake pamoja na kuendelea kuwekeza kwa waamini
walei, ili wasaidie mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Kanisa pale linapoweza
linatoa pia msaada na mikopo nafuu kwa ajili ya kukuza maendeleo ya watu.
Kwa
njia ya majiundo makini ya kulinda na kutunza mazingira, kwa kuwekeza kikamilifu katika
kilimo cha kisasa na endelevu; kwa kuwapatia wakulima mtaji na pembejeo za kisasa
sanjari na kuzingatia haki zao msingi, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa na uhakika
wa usalama wa chakula na maendeleo ya watu. Kanisa litaendelea kuwekeza katika huduma
kwa maskini kama sehemu ya utekelezaji wa utume wake kwa maskini na kwa ajili ya maskini.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.