2015-02-21 16:10:14

Kumbatieni Injili ya Uhai!


Jimbo Katoliki la Cassano Jionio linaongozwa na Askofu Nunzio Galantino ambaye pia ni Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia lina utajiri mkubwa wa tamaduni na Mapokeo mbali mbali; mambo ambayo yanalitajirisha Kanisa. Jumuiya ambayo imekuwa ikijitahidi kumwilisha mshikamano wa upendo kwa watu wanaobisha hodi Jimboni humo kwa kutambua kwamba, upendo, ukarimu na huruma hii, wanamfanyia Kristo anayejionesha kwa njia ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ukarimu wa upendo ni huduma ya kichungaji inayofanywa na Jumuiya ya Emmanuel kwa kujikita katika maisha ya sala na tafakari ya Neno la Mungu; mahali pa familia kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana ndani na nje ya Italia. Itakumbukwa kwamba, hii ni Jumuiya ambayo hivi karibuni ilitembelewa na Baba Mtakatifu Francisko, akapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wafungwa, wagonjwa; wakleri, watawa na majandokasisi; tukio ambalo lilimwezesha kuona ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma.

Changamoto kubwa iliyoko mbele yao kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuwa ni Jumuiya inayijipambanua kwa ukarimu ili kuwasaidia watu kutambua uwepo wa Kristo unaoponya na kukomboa. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 21 Februari 2015 wakati alipokutana na kuzunguza na Familia ya Mungu kutoka Jimbo Katoliki la Cassano Jonio.

Baba Mtakatifu Francisko anasema mtu anayempenda Yesu na kusikiliza maneno yake kwa kuishi katika ukweli na uwazi, hawezi kamwe kuogelea katika matendo maovu. Wakristo hawana budi kuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; wawe ni vyombo vya haki, amani na utulivu pamoja na kusaidia kulinda na kutunza mazingira. Huu ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuimarisha uhusiano mwema na Yesu Kristo pamoja na Kanisa lake. Ukristo uoneshwe kwa njia ya ushuhuda wa matendo adili, kwa kujikita katika utawala wa sheria na kutenda haki.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wote wanaoogelea katika dhambi na matendo maovu yanayomchukiza Mungu na jirani, kufanya toba na kufungua mioyo yao ili kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwani Mama Kanisa anawasubiri kwa upendo na huruma, ili kuwasaidia kutenda mema. Ardhi nzuri ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, rasilimali inayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa kwa ajili ya mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho, changamoto inayoapaswa kufanyiwa kazi na Serikali kwa kushirikiana na wananchi wake.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wanachama wa Jumuiya ya Emmanuel wanaowapokea na kuwaonjesha upendo na ukarimu maskini na wanyonge. Hawa ni vijana waliokuwa wanatumia dawa haramu za kulevya, lakini sasa wanahifadhiwwa kwenye taasisi ya Msamaria mwema, iliyothubutu kujinyenyekesha ili kuwatibu na kuwaganga vijana hawa, kiasi cha kuzirudishia tena familia nyingi matumaini yaliyokuwa yameanza kuyeyuka kama ndoto ya mchana. Mama Kanisa anatambua mchango na huduma inayotolewa na Jumuiya hii kwa ajili ya maskini kwa kumpokea Kristo na kuendelea kupandikiza mbegu ya matumaini kwa wale waliokata tamaa na kupondeka moyo.

Baba Mtakatifu anasema, ulimwengu mamboleo unahitaji kuonjeshwa matumaini. Vijana wengi wanaweza kujikuta wakishindwa kuwa na matumaini kutokana na matatizo pamoja na machungu ya maisha; hawa wanapaswa kuonjeshwa matumaini kwa njia ya ukarimu na mapendo, ili kuwaamshia tena matumaini mapya. Jumuiya za Kikristo hazina budi kuwa kweli wadau wa mshikamano wa upendo dhidi ya watu wanaopandikiza mbegu ya ubinafsi, chuki na ukosefu wa haki.

Waamini washinde kishawishi cha kukumbatia utamaduni wa kifo, kwa kuwa ni mashuhuda amini wa Injili ya Uhai. Mwanga wa Neno la Mungu uwe ni dira na mwongozo wa maisha kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili awasaidie kuona na kuwajibika katika mapambano ya mifumo mipya ya umaskini mamboleo, unaodhalilisha utu na heshima ya vijana na familia nyingi duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.