2015-02-21 16:26:40

Kuhusu akiba ya uzeeni? Ni kicheko tupu!


Viongozi watendaji wa Mfuko wa Akiba ya Uzeeni wa Vatican katika kikao chake kilichohitimishwa hivi karibuni unasema kwamba, habari zilizokuwa zimezagaa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuhusu ukata ulioukumba Mfuko huu kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na majukumu yake kwa siku za usoni, si kweli ni uzushi mtupu.

Taarifa ya fedha iliyopitishwa na Sekretarieti kuu ya Vatican inaonesha kwamba, hali ni nzuri na wala hakuna sababu kwa wafanyakazi wa Vatican kuhofia malipo yao ya uzeeni kwa siku za usoni. Taarifa ya fedha imepitiwa na kuthibitishwa pia na Baraza la Mfuko wa Akiba ya Uzeeni wa Vatican inaonesha kwamba, kumekuwepo na ongezeko la mchango wa wafanyakazi kwa asilimia 26% hata baada ya kuongeza muda wa miaka miwili kwa wafanyakazi kwenda pensheni, yaani wafikiapo miaka 67 kwa wafanyakazi walei na kwa Wakleri na Watawa wafikiapo miaka 72.

Takwimu zinaonesha kwamba, hali ya mfuko ni nzuri na kwamba una rasilimali ya kutosha kuweza kugharimia akiba ya uzeeni kwa wafanyakazi wa Vatican wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa Kanisa. Mfuko unaonesha kwamba, unaweza kukabiliana na gharama za malipo kwa asilimia 95% na kwamba, pato la mfuko linaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na faida inayopatikana kutoka kwenye vitega uchumi vyake.

Taarifa inaonesha kwamba, kuanzia mwaka 1993 hadi mwaka 2013 kumekuwepo na ongezeko la Euro 22, 256, 196 kwa mwaka. Katika kipindi cha miaka sita iliyopita kumekuwepo na ongezeko kutoka kiasi cha Euro 23, 583, 882 hadi kufikia Euro 26, 866, 657, kiasi cha fedha kinachotosha kugharimia pensheni kwa wafanyakazi wa Vatican kwa sasa.

Taarifa ya Mfuko wa akiba ya uzeeni inaonesha kwamba, hadi kufikia tarehe 31 Desemba 2014 mfuko ulikuwa na rasilimali yenye thamani ya Euro 477, 668, 000 na kwamba, kwa mwaka 2015 kutakuwa na salio la Euro 27, 140, 000. Rasilimali na vitega uchumi vyake vyote ni sawa na zaidi ya Euro millioni 504, hali inayoonesha kwamba, Mfuko wa akiba ya uzeeni Vatican unaendelea kufanya vyema kwa kuzingatia kanuni maadili, ukweli na uwazi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.