2015-02-21 16:19:23

Jitahidini kujipatanisha na Mungu na jirani!


Kipindi cha Kwaresima kiwasaidie waamini kusali kwa bidii na uchaji; kufunga na kujinyima kwa ajili ya kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na udugu; kutubu na kumwongokea Mungu na jirani, ili kuweza kukamilisha hija ya Kipindi cha Kwaresima na hatimaye, kusherehekea Fumbo la Pasaka kwa mioyo safi! Ni changamoto inayotolewa na Kardinali Mario Aurelio Poli wa Jimbo kuu la Buenos Aires.

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia unaogubikwa na tabia ya ukanimungu, hata Wakristo wanajikuta wakiwa na imani haba kama "kiatu cha raba", watu wanaoishi na kutenda kana kwamba, hakuna tena maisha baada ya kifo. Hata waamini wanajikuta wakimezwa na ile falsafa ya "ponda mali kufa kwaja" au "vunja mifupa ungali na meno". Mwenyezi Mungu kwa kuutambua udhaifu na mapungufu ya binadamu, amemwekea Kipindi cha Siku Arobaini, yaani Kwaresima, ili kukimbilia upendo na huruma ya Mungu kwa kutubu na kuiamini Injili.

Kardinali Poli anasema, si haba kuona watu wanafunga na kujinyima kwa ajili ya kutafuta ulimbwende, ili waonekane na kupendwa. Kuna watu wengi ambao duniani wanafunga kwa takribani mwaka mzima, kwa kupata mlo kiduchu; njaa na mateso kwao kimekuwa ni chakula cha kila siku, kufunga ni sehemu ya maisha yao kutokana na shida wanazokabiliana nazo. Lakini kwa Mkristo, anaalikwa kufunga na kujinyima wakati huu wa kipindi cha Kwaresima, ili kuwasaidia watu wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na baa la njaa na utapiamlo duniani. Wakristo wajifunze kujinyima kwa ajili ya kuwasaidia jirani zao wenye shida na mhangaiko zaidi. Ni kujisadaka kwa kuzingatia haki na kutenda wema kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Kardinali Poli anasema, kile kidogo ambacho mwamini amejinyima kwa ajili ya mfungo wa Kwaresima, kisaidie katika utekelezaji wa matendo ya huruma na upatanisho kati ya Mungu na binadamu. Kwaresima kiwe ni kipindi kinachomsaidia mwamini kujipatanisha na nafsi yake mwenyewe, kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zake, ili kwa wote kwa pamoja waweze kumwimbia Kristo wimbo wa sifa na utukufu wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Pasaka.

Waamini wanakumbushwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, walau wanaungama mara moja kwa mwaka hasa wakati wa Pasaka. Kwa njia ya mwaliko huu, waamini wajenge utamaduni wa kujipatanisha na Mungu mara kwa mara, lakini kwa namna ya pekee wakati huu wa Kwaresima, yaani katika kipindi cha Siku arobaini, wasingoje dakika za mwisho wakati wa Juma kuu! Waamini watumie kipindi hiki kukimbilia upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Ni kipindi cha kuachana na kinzani na misigano isiyokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka huu uliotiwa mkwaju na Askofu mkuu Josè Maria Arancedo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina anakazia umuhimu wa waamini kujenga na kudumisha mchakato wa toba na wongofu wa ndani unaojikita katika ari na moyo wa kimissionari. Lengo ni kutekeleza dhamana na wajibu wa kila mwamini kwa umakini, weledi, juhudi na maarifa. Waamini wawaonjeshe na kuwashirikisha jirani zao ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo.

Kipindi cha Kwaresima kiwasaidie waamini kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kuondokana na ubinafsi na uchoyo, tayari kuanza mchakato wa kutafuta na kukumbatia utakatifu wa maisha unaojikita katika toba. Wakristo wanahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kutoka kifua mbele, ili kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya matendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.