Ifuatayo ni tafakari ya Njia ya Msalaba, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Kipindi
cha Kwaresima, muda wa kusali, kutafakari, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Chukua
muda kidogo, ili uweze kuitafakari kwa ajili ya ustawi wa maisha yako ya kiroho! Ukitaka
mshirikishe pia jirani yako kwa njia za mitandao ya kijamii, kwani kizuri, kinaliwa
na wengi! KITUO CHA KWANZA YESU ANAHUKUMIWA AFE.. (Matayo 27:11 - 26) Ee
Bwana Yesu Kristo tunakuabudu na kukushukuru.... Pilato anamuhukumu Yesu bila kosa
lo lote. Utawala, sera, siasa si msaada kwa Yesu mnyonge. Nasi pia kuna nyakati ambazo
mahakama, serikali, familia, utawala au hata rafiki zetu wapendwa na wenzetu wa ndoa
waweza kuwa si msaada kwetu. Tutajikuta tupo peke yetu tumetelekezwa na kukosa pa
kuegemea. Dunia yote itaninyooshea vidole mimi peke yangu. Utaonja hali ya kuwa mpweke
ukawa wewe na Mungu wako tu. Utajiuliza, hata mume wangu wa ndoa au hata mke wangu
ananisaliti mbele ya ndugu zake ? Wangapi wana uchungu moyoni na akilini kwa kubambikiziwa
kesi za kusingiziwa mahakamani ? Wangapi tumebeba aibu na machungu ya kuuzwa hivi
hivi kama Yusufu Misri na ndugu wa tumbo moja ? (Mwanzo 37:12 - 36). Wangapi tumetendewa
vibaya kwa kutopewa nafasi ya kusikilizwa na wenzetu wa ndoa tunapotofautiana ndani
ya familia ? Baba anarudi jioni na kufoka tu kama mbogo na kuhukumu kwa dogo nililofanya
nyumbani. Huenda nimetoa tu fulana moja iliyochakaa ya baba kwa kijana wa shamba (shamba
boy) na moja kwa moja baba anafoka na kusema mimi natembea na kijana huyo. Hadhi yangu
yote ya kuwa mimi ni mke wake kwa miaka 15 na kumzalia watoto watatu wazuri inaporomoka
kwa dakika moja. Wangapi tumefukuzwa kazi kiholela makazini bila ya kufuata tararibu,
sheria na miongozo ya kazi ? Kazini kumekuwa ni sehemu za kusikiliza majungu tu, au
nani wa kwanza kaenda kwa bosi na si kuangalia ukweli wa tatizo. Sisi sote makazini
tunajiona ni kama mbuzi wa kafara tu. Kazi zinagawiwa au vyeo vinapandishwa kwa kuangalia
dini, ukabila, urafiki, undugu au hata maelekeo yanayoashiria mapenzi na ngono. Hakuna
vigezo vya elimu au uzoefu. Uongozi si dhamana tena kwa niaba ya wanyonge. Viongozi
wetu ni kama Pilato. Ni viongozi wa kuangalia upepo au ushabiki wa siku husika kama
ule wa Yanga na Simba. Uongozi unaangalia maslahi hewa ya kelele za watu wa wakati
husika. Macho ya Pilato yanafumbwa kwa kutoona mbele. Ukweli kwake si kitu chenye
mashiko. Anatetea urafiki wa muda na Kaisari. Uongozi hausimamii tena haki, ukweli,
bali ni woga mtupu. Pilato na majeshi yake yote anashindwa kusimama kwa miguu yake. Wapendwa
Wagetsemani, siku ya leo katika kituo cha kwanza tusali na kuomba kwa ajili ya wale
wanaotendewa ubaya huu wa kuhukuniwa bila kosa. Tuombe : Ee Bwana Yesu uliyehukumiwa
bila kosa lo lote, wajalie viongozi wetu waweze kusimamia maamuzi yao kwa miguu yao
wenyewe. Vijalie vyombo vinavyosimamia sheria na haki, hasa mahakimu na majaji ili
waweze kuhukumu kesi mbali mbali kwa haki na ukweli. Jalia familia zetu ziwe na nafasi
ya unyenyekevu wa mazungunzano pale panapotokea shida au tofauti ili ukweli uonekane
na kufikiwa muafaka wa kindugu na Kikristu. Kwaresima njema wapendwa, Fr Benno
Kikudo, Jimbo kuu la Dar es Salaam.