2015-02-20 14:53:11

Sikilizeni kwa makini sauti za waamini wenu!


Kuna uhusiano wa pekee unaojengeka katika msingi wa udugu na urafiki kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa la Ukraine ambalo lina utajiri mkubwa na amana ya Kanisa inayojidhihirisha katika Mapokeo. Hii ni nchi ambayo kwa sasa inakabiliwa na kinzani na changamoto za maisha, lakini Kanisa lina mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu nchini Ukraine.

Vita na kinzani za kijamii zinaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Ni kinzani ambazo zinafumbatwa katika sera za kisiasa ambazo kwa bahati mbaya, Kanisa haliwezi kuzitolea maamuzi, lakini Kanisa linaweza kuchangia katika ustawi na maendeleo ya watu, kwa kuwa na mwelekeo chanya zaidi. Kanisa linaendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani, ili wadau wote waweze kupata ujasiri wa kuweka silaha zao chini na kuanza mchakato wa majadiliano; kwa kueshimu mkataba wa kusitisha vita uliotiwa sahihi hivi karibuni na kushuhudiwa na Jumuiya ya Kimataifa, kama hatua muhimu sana ya kudumisha amani.

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 20 Februari 2015 alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Ukraine, linalofanya hija ya kitume hapa mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kusikiliza kwa makini sauti ya waamini wao, ili waweze kujikita katika mchakato utakaowakutanisha, washirikisha na kuwajengea uwezo wa kupembua kwa kina na mapana kinzani, ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, kwani kuna uwezekano mkubwa wa kutafuta amani na ikapatikana kweli.

Baba Mtakatifu anawakumbusha Maaskofu wa Ukraine kwamba wao wana amana inayojikita katika maadili na upendo; mambo ambayo yanabubujika kutoka katika Mapokeo ya Kanisa. Maaskofu ni raia kama raia wengine wowote, kumbe wanaweza kuchangia mawazo na tunu msingi ambazo zitachangia ujenzi wa mfungamano wa kijamii nchini Ukraine pamoja na kuendeleza mafao ya wengi. Vatican kwa upande wake imeionesha Jumuiya ya Kimataifa msimamo wa Kanisa unaojikita katika tunu msingi za Kiinjili na mikakati ya kichungaji ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto nyingi za kisheria.

Vita inayoendelea nchini Ukraine imesababisha mpasuko wa kifamilia pamoja na kuwa na mwelekeo tenge wa uhuru wa kiuchumi, uliopelekea baadhi ya wananchi kufaidika na kuwaacha wananchi wengi wakiwa wanaogelea katika mateso na mahangaiko na umaskini mkubwa katika nchi ambayo ina ukarimu na utajiri mkubwa.

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu wa Ukraine kuwasaidia waamini wao kujenga na kudumisha imani, haki, ukweli na maadili katika medani mbali mbali za maisha. Kama viongozi wa Kanisa hawana budi kuwa huru na hata katika umaskini wao, wajikite katika kulinda na kutetea familia na maskini; wanyonge na watu wasiokuwa na ajira; wagonjwa na wazee; walemavu na watu wasiokuwa na makazi maalum.

Maaskofu waendelee kuwatangazia Watu Injili ya Matumaini; washirikiane na kusaidiana katika kukuza na kudumisha miito mitakatifu kwani mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Maaskofu wakazie majiundo makini ya Wakeri na Watawa, ili hatimaye, waweze kutoa huduma makini inayojikita katika imani kwa ajili ya Watu wa Mungu.

Maaskofu wajenge na kuimarisha umoja na mshikamano kati yao hata katika utofauti wa madhehebu wanayotumia. Pale kunapotokea misigano na migawanyiko, wasisite kumkimbilia Yesu, ili aweze kuwaganga na kuwaponya majeraha yao, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Watu wa Mungu sanjari na kuendeleza majadiliano ya kiekumene, ili Wakristo waweze kushirikiana kwa dhati.

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu kwa kuwa karibu na kutembea pamoja nao katika maisha yao ya kila siku bila kusahau kushirikiana na viongozi wa Serikali kwa ajili ya mafao ya wengi, kwani wao ni vyombo vya umoja na unabii; mwaliko wa kuliendeleza Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican







All the contents on this site are copyrighted ©.