2015-02-20 09:48:32

Pandisheni bendera ya upendo!


Baraza la Maaskofu Katoliki kutoka Ukraine, Alhamisi, tarehe 19 Februari 2015 limeadhimisha Ibada ya Masifu ya Jioni, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma, kwa ajili ya kuombea amani, utulivu na ustawi nchini mwao wakati huu wanapofanya hija ya kitume mjini Vatican, inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano. Ibada hii imehudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Vatican pamoja na Familia ya Mungu nchini Ukraine.

Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lina umuhimu wa pekee sana kwa Wakristo wa Makanisa ya Mashariki, kwani hapa wanaweza kuona mwanga wa imani na matumaini katika mateso na mahangaiko yao ya ndani; ni mahali wanaposali na kumkimbilia Mwenyezi Mungu kwa njia ya maombezi ya Bikira Maria; hapa ni mahali panapowachangamotisha waamini kuendeleza mchakato wa upatanisho, haki na amani bila kuchoka wala kukata tamaa hata kama cheche za amani ya kweli bado hazijaanza kuonekana. Bikira Maria ni kielelezo amini cha wafuasi wa Kristo, aliyethubutu kuyaweka yote moyoni mwake, akawa kweli ni kielelezo na mfano wa kuigwa katika imani, matumaini na mapendo.

Ni maneno yaliyotolewa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki wakati wa Ibada ya Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Bikira Maria aliteseka sana moyoni mwake kumwona Mwanaye wa pekee akiwa ametundikwa Msalabani; akaonesha furaha ya ajabu aliposikia kwamba Mwanaye mpendwa amefufuka kutoka katika wafu, hapo akatambua kwamba, kweli Mwenyezi Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake.

Kwa njia ya maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, hakuna tena kizingiti, vita, kinzani na migawanyiko inayoweza kufunga lango la matumaini, kwani Kristo ameshinda mauti na Yeye ndiye chemchemi ya imani ya Kanisa. Bado waamini wanaalikwa kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa, ili vita ambayo imekuwa ni chanzo cha majanga makubwa kwa wananchi wa Ukraine iweze kukoma.

Kardinali Sandri anawapongeza wananchi wa Ukraine kwa moyo wa upendo, sadaka na majitoleo yao ambayo yamewezesha kuchangia kwa hali na mali, ili kuwasaidia wananchi wa Ukaraine wanaoteseka kutokana na vita. Anawashukuru Wasamaria wema ambao wanaendelea kuchangia kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Ukraine.

Watu watambue kwamba, chuki, uhasama na vita ni mambo yanayoharibu na kamwe hayatasaidia mchakato wa ujenzi na maendeleo ya watu, changamoto na mwaliko wa kujiondoa kutoka katika mazingira na mambo yote yanayoweza kuwa ni sababu ya chuki na uhasama kati ya watu, tayari kujikita katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Wananchi wathubutu kupandisha bendera ya upendo dhidi ya chuki na vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.