2015-02-20 14:56:06

Msimtumie Mungu kuhalalisha maovu!


Wakristo katika kipindi hiki cha Kwaresima wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha upendo kwa Mungu na jirani kwa njia ya matendo ya huruma. Ni mwaliko wa kuzingatia haki na kutenda mema na kwamba, imani ijidhihirishe katika matendo mema. Ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, siku ya Ijumaa, tarehe 20 Februari 2015.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufunga na kusali; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha unaoleta mabadiliko kutoka katika undani wa mtu! Mafarisayo walikuwa ni wepesi wa kuonesha matendo ya nje lakini ndani walikuwa ni wanafiki wakubwa. Upendo kwa Mungu na jirani ni sawa na chanda na pete; tunu msingi inayomwezesha mwamini kufanya toba na wongofu wa ndani.

Yesu anawaalika wafuasi wake kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, kuwafungulia wafungwa na wote waliosetwa; kuwavisha walio uchi na kutenda haki. Baba Mtakatifu anasema hii ndiyo funga ya kweli. Upendo kwa Mungu na jirani ni muhtasari wa Amri kuu za Mungu kama zinavyobainishwa kwenye Maandiko Matakatifu na kikolezo muhimu sana cha toba na wongofu wa ndani.

Baba Mtakatifu anasema ni dhambi kubwa kumtumia Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuficha dhambi zako, kwani imani inapaswa kuoneshwa katika matendo. Wakuu wa na wasimamizi wa kazi wanapaswa kuzingatia haki na kutenda mema, kwa kulipa mishahara ya haki kwa wafanyakazi wao, kuwakatia bima ya afya pamoja na kuhakikisha kwamba, wanayo malipo ya akiba ya uzeeni. Upendo hauna budi pia kuanzia ndani ya familia, ili uweze kuenea na kusambaa kwa majirani.

Kwaresima ni hija inayofanywa na mwamini ili kumwendea Mwenyezi Mungu na jirani na wala si kwa kuzingatia sheria na maagizo ya Kanisa pasi na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha, kwani imani ya kweli inashuhudiwa katika matendo. Waamini wajifunze kutenda kwa haraka na kwa kuzingatia maadili na kanuni za kazi.

Kwaresima ni kipindi cha kutoa nafasi ili kuwapokea wale ambao wamewakosea na kuwatendea jeuri ili kuwaonjesha tena huruma na upendo wa Mungu; wagonjwa na maskini; wazee na watoto yatima. Watu wote hawa wanahitaji kuonja mwanga na matunda ya funga ya Kwaresima. Ni wakati wa kuwakumbuka na kuwaombea wafungwa ili waweze kubadili mioyo na maisha yao, wagonjwa waweze kupona kurudi tena majumbani mwao. Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.