2015-02-20 09:45:08

Mshikamano wa dhati na wakimbizi!


Kardinali Bechara Rai, Patriaki wa Kanisa la Wamoniti nchini Lebanon katika ujumbe wake wa Kipindi cha Kwaresima anawaomba Wakristo kuonesha mshikamano wa upendo na udugu kwa wahamiaji na wakimbizi kutoka Syria na Iraq wanaohifadhiwa nchini Lebanon.

Ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka 2015 kutoka kwa Patriaki Rai unajikita katika mada ya mshikamano wa upendo, kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anaihamasisha Familia ya Mungu kuondokana na utamaduni usioguswa na mahangaiko ya watu na badala yake kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano wa kidugu, watu wanaoteseka, kudhulumika na kunyanyasika sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha walimwengu kwamba, kamwe Mwenyezi Mungu hajawageuzia kisogo, kwani anawapenda kiasi hata cha kumtoa Mwanaye wa pekee, Yesu Kristo ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utilimifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo, Mwenyezi Mungu ameweza kutengeneza daraja la mawasiliano kati yake na binadamu. Yesu Kristo Mungu kweli na Mtu kweli ndiye kiungo muhimu kati ya Mungu na binadamu.

Kardinali Rai anasema kwamba, Kanisa ni kama mkono unaofungua lango la mawasiliano na mahusiano mema kati ya Mungu na binadamu, kwa njia ya utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu; katika Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na katika kuendeleza mchakato wa ushuhuda wa imani katika matendo ya huruma. Hata pale dunia inataka kujifungia katika undani wake kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka huu, lakini Mwenyezi Mungu bado anaendelea kujitaabisha kumtafuta mwanadamu.

Hapa jambo la msingi kwa waamini ni kufanya toba na wongofu wa ndani, kwa kuwaonjesha upendo na mshikamano wa dhati maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwa namna ya pekee wakimbizi na wahamiaji huko Syria na Iraq. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wasaidia kuchangia kwa hali na mali shughuli zinazofanywa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Lebano, Caritas Lebanon, ili liweze kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ambao wanateseka sana kutokana na vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati. Wakristo watambue kwamba, hata kama ni mali ya binafsi, lakini daima inapaswa kusaidia mchakato wa kukuza na kuendeleza ustawi na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.