2015-02-19 09:06:15

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya kwanza ya Kwaresima


Mpendwa mwana wa Mungu, ninakusalimu nikisema tumsifu Yesu Kristo. Ninatumaini uko tayari kupokea ujumbe wa Neno la Mungu kwa furaha. Tuko tayari katika kipindi cha kwaresima kipindi cha toba ambapo Mama Kanisa anatualika kujiweka tayari kwa njia ya toba kuenenda tena katika uzima mpya tulioupokea wakati wa ubatizo. RealAudioMP3

Kipindi cha Kwaresima, ni kipindi ambacho chatuweka tayari kwa Fumbo la Pasaka. Ni kipindi cha mapinduzi ya kiroho, mapinduzi ya ndani, yaani kumtafuta Mungu zaidi kwa kuyatimiza mapenzi yake. Mazoezi yote ya kiroho, kujinyima raha za kidunia, kufunga chakula ni namna ya kuunganika na Kristu mteswa hadi ufufuko wake.

Ni kwa lengo la kubadili maisha yetu ya ndani, Neno la Mungu Dominika ya kwanza latuambia kuwa Mungu anaanzisha hali mpya ya maisha, yaani utu mpya, toka mafuriko tokeo la dhambi kuelekea maisha mapya.

Katika somo la kwanza tunapata kusikia habari juu ya mafuriko ya Noa. Kwa hakika jambo hili linatisha sana na laweza kuonesha na kutufikirisha kuwa Mungu hatupendi na hivi anapenda angamizo hilo. Badala yake Mungu ni mwema daima! Jambo la mafuriko ni tokeo la kiburi chetu na dhambi zetu sisi wenyewe. Kumbe, Mungu anaingilia kati na anaanzisha utu mpya, familia mpya na anahaidi baraka na mambo mapya na kamwe hakutakuwa na angamizo jingine kama hilo. Hili ndilo agano ambalo Mungu anafanya na watu. (Mw. 9: 9-11) Upendo wake unaojionesha katika agano hauna masharti bali ni huruma kamilifu itokayo katika mtima wake ambayo yaleta maisha mapya na mabadiliko mioyoni mwa watu.

Mtume Petro katika barua yake ya I sura ya III anapowaandikia watu wote anatupeni habari njema iletwayo na Yesu Kristu Mwana wa Mungu. Anasema kwa njia ya Yesu ambaye hakuwa na dhambi, wote waliokuwa na dhambi yaani wasiokuwa haki wameweza kuokoka. Ni kwa njia ya mauti ya msalaba sote tumekombolewa. Amevunjilia mbali kiburi ambacho kilileta mafuriko katika Agano la kale, ameleta maisha mapya kwa mwanadamu. Kristu ndiyo huruma ya Mungu, ndiye limbuko la wote waliokuwa wamezama katika dhambi. Kama ambavyo Kristo ameenda zake mbinguni nasi kwa njia yake tukiitikia utume wake hapa duniani tutaingia mbinguni.

Sehemu ya Injili ya Marko 1:12-15 inaanzisha safari nzima ya Kwaresima, inakualika kutubu yaani kuungama dhambi zako mbele ya Mungu ili uweze kupokea ujumbe wa Neno lake daima. Kwa njia ya toba tunaweza kupata nafasi ya kuamini na kusadiki kina mafundisho yote ya Yesu Kristo mteswa na mchungaji mwema. Toba ni mlango wa neema na imani yetu ni mlango wa umisionari. Wajibu huu ni mgumu lakini Kristu mwenyewe ametupa mfano kamili, amejaribiwa na ameonja ugumu katika safari yake ya kuokoa ulimwengu.

Bwana yuko jangwani kwa siku 40 akisali na kutafakari kuhusu mapenzi ya Mungu. Katika jangwa anajaribiwa lakini anasonga mbele bila kuogopa wala kukata tamaa. Jambo hili latufundisha kuwa, tunapoanza safari ya wokovu kwa njia ya ubatizo tunapata Roho wa Mungu wa kutusaidia katika safari, hata hivyo hatukingiwi majaribu bali tunaalikwa kukabiliana nayo kwa unyenyekevu jangwani tukitafakari kwa furaha mapendo ya Mungu.

Yesu hakukaa jangwani kwa siku moja bali siku 40 zikimaanisha maisha yake mazima, ndiyo kusema nasi twapaswa kusali na kuomba maisha yetu yote. Jangwa ni alama ya nguvu pinzani na hivi tunapobatizwa imani haiwi jambo la lelemama bali ni shughuli pevu ambayo tunapaswa kuitenda siku kwa siku sasa na mpaka mwisho wa maisha yetu hapa duniani.

Mpendwa mwana wa Mungu, ninakutakieni kwaresima njema na maisha ya toba daima, ili kwa njia hiyo uweze kupokea imani na msamaha wa dhambi na kwa namna hiyo kukaa tayari kupokea mavuno mwishoni mwa Kwaresima lakini hasa uzima wa milele.

Toka Radio Vatican mimi ni Pd Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.