2015-02-19 09:34:16

Salam za rambi rambi!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kufuatia taarifa za kifo cha Askofu Mstaafu Magnus Mwalunyungu wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi aliyefariki dunia tarehe 12 Februari, 2015 katika Hospitali ya Tosamaganga iliyoko Jimbo Katoliki la Iringa alikokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa Tosamaganga, Jimbo Katoliki la Iringa, Ijumaa, tarehe 20 Februari, 2015.

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za kifo cha Askofu Mstaafu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Tunduru – Masasi katika Mkoa wa Mtwara, Marehemu Baba Askofu Magnus Mwalunyungu ambacho nimejulishwa kuwa kimetokea usiku wa kuamkia tarehe 13 Februari, 2015 katika Hospitali ya Tosamaganga, Iringa alikokuwa amelazwa kwa matibabu”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.

Aidha Rais Kikwete amesema Marehemu Baba Askofu Mwalunyungu, enzi za uhai wake, alikuwa miongoni mwa Watumishi hodari wa Kiroho aliyewatumikia waamini wake wa Kanisa Katoliki kwa bidii kubwa tangu alipopata Daraja la Upadre mwaka 1959, na kwa miaka mingi akaiongoza Seminari Kuu ya Kipalapala iliyoko Jimbo kuu la Tabora.

Aidha Rais Kikwete amesema kifo cha Askofu Mwalunyungu kimelifanya Kanisa Katoliki lipoteze Kiongozi Shupavu wa Kiroho, kwani ingawa alikuwa amestaafu, Utumishi wake wa Kiroho kwa Kanisa Katoliki na Waamini wa Kanisa hilo kwa ujumla, ulikuwa bado unahitajika sana hasa katika nyanja za ushauri na maelekezo.
“Naomba mpokee salamu zangu za rambirambi kwa kumpoteza Baba Askofu Magnus Mwalunyungu, na naomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Roho yake Mahala Pema Peponi, Amina”, amemalizia kusema Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi.








All the contents on this site are copyrighted ©.