2015-02-19 09:16:15

Mnafiki hana machozi wala huruma!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jumatano ya Majivu, tarehe 18 Februari 2015, mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, yaani muda muafaka kwa waamini kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, toba na tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma, ameongoza maandamano ya toba kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anselmi lililoko mjini Roma hadi kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina. Ibada hii imehudhuriwa na Familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma.

Baba Mtakatifu baada ya maandamano ya toba, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu ambamo waamini wamepakwa majivu, alama ya toba kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Baba Mtakatifu amepakwa majivu na Kardinali Josefu Tomko na baadaye Baba Mtakatifu aliendelea kuwapaka majivu Makardinali na Maaskofu waliokuwa wamehudhuria Ibada hii ya Misa Takatifu. Kipindi cha Kwaresima ni mwaliko kwa Familia ya Mungu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na kufunga.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amejikita zaidi katika Kitabu cha Nabii Yoeli anayewataka Waisraeli kumrudia Mwenyezi Mungu kwa moyo wote; maana yake kwa kuanzisha mchakato wa toba ya ndani inayomshirikisha mwamini mmoja mmoja na jumuiya yote, kwa kuwataka Makuhani kuwasindikiza Watu wa Mungu kwa machozi na maombolezo makuu.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, anawaalika viongozi wa Kanisa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia neema ya kulia na kuomboleza katika sala, toba na wongofu wa ndani; kwa kufanya malipizi ya kweli pasi na unafiki, kwa kutambua kwamba, mnafiki kamwe hawezi kutoa machozi kutoka katika undani wa moyo wake. Kwaresima kiwe ni kipindi cha kusali, kufunga, kutenda wema na haki katika hali ya usiri pasi ya kutaka kuonekana na watu kwani kwa kawaida watu wanapenda kuonekana wanapotenda mema, lakini Yesu anawaalika wafuasi wake kufanya yote haya kwa siri kwani Baba yao aliyeko sirini anatambua yote.

Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, anayeendelea kuwaalika waja wake kumgeukia kwa moyo wa toba na majuto. Yesu Kristo kwa namna ya pekee, anawataka waamini kujipatanisha na Mwenyezi Mungu bila kusahau kujipatanisha na jirani zao; jambo ambalo linawezekana kutokana na huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake, kiasi hata cha kumtoa Mwanaye wa pekee ili aweze kuwa ni fidia ya wengi, akateswa na hatimaye, akafa Msalabani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linakianza kipindi hiki cha Kwaresima likiwa na matumaini kwa Bikira Maria, Mama asiyekuwa na doa la dhambi, atawasaidia watoto wake katika mapambano dhidi ya dhambi, ili hatimaye wakati wa Siku kuu ya Pasaka, kwa pamoja waweze kumwimbia Mwenyezi Mungu wimbo wa ushindi wa Kristo.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini maneno ya kubariki majivu kwa kusema kwamba, binadamu ni mavumbi na mavumbini atarudi tena; tubuni na kuiamini Injili. Hapa waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni viumbe wadhambi wanaohitaji toba na wongofu wa ndani, changamoto kubwa kwa walimwengu mambo leo. Toba na wongofu wa ndani unamwezesha mwamini kurudi na kuonja tena huruma na upendo wa Mwenyezi Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu aliyejidhaminisha mikononi mwa Baba mwenye huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.