2015-02-19 12:03:44

Chagueni maisha ili mpate kuishi!


Katika hali na mazingira mbali mbali ya maisha, mwamini anapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu sanjari na kuhakikisha kwamba, anajiondoa katika mazoea na mazingira ambayo ni makwazo katika mchakato wa ujenzi wa mahusiano mema na Mwenyezi Mungu. Kwa kumchagua na kumpatia Mungu kipaumbele cha kwanza ni kwa kumwabudu na kumtukuza badala ya kumezwa na malimwengu.

Katika Liturujia ya Neno la Mungu, Alhamisi, tarehe 19 Februari 2015, Mwenyezi Mungu anamwambia Musa kwamba amemwekea mbele uzima na mema, mauti na mabaya na kumwamuru kuenenda katika njia za Mungu na kushika maagizo, amri na hukumu zake ili apate kuwa hai na kuongezeka.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Kipindi cha Kwaresima. Musa aliamua kuchagua mema na kuenenda katika njia za Bwana, changamoto na mwaliko hata kwa Wakristo wa nyakati hizi, kwa kuondokana na mazoea na mambo ambayo yanagumisha mahusiano mema na Mwenyezi Mungu. Kunahitaji moyo na ujasiri wa kuweza kuchagua na kutenda mema kwani huu ndio ushauri ambao Mwenyezi Mungu anautoa kwa waja wake kwa wakati huu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuchunguza dhamiri zao na kuangalia mahusiano yao na Mwenyezi Mungu, ndani ya familia na jamii katika ujumla wake. Yesu anawaonya wafuasi wake katika Injili ya leo kwamba, yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe? Kwa mtu anayetafuta mambo yake mwenyewe atambue kwamba, amepoteza dira, njia na mwelekeo na matokeo yake ni kilio na kusaga meno.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, ikiwa kama wanataka kufanya maamuzi yenye uhakika hawana budi kumshirikisha Mwenyezi Mungu, kwa kumwomba ili awasaidie kupata neema wanayohitaji ili kufanya maamuzi ya kijasiri, kwa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Hapa waamini watambue kwamba, daima watapata msaada wa Mungu kwani hawezi kuwaacha pweke, lakini, jambo la msingi ni mwamini mwenyewe kuonesha imani na matumaini kwake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.