Patriaki Louis Sako wa Kanisa la Babilonia ya Walkadei, katika ujumbe wake kwa Kipindi
cha Kwaresima anasema, huu ni muda muafaka uliokubalika mbele ya Mwenyezi Mungu wa
kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa nchini
Iraq. Kiwe ni kipindi cha kujisomea, kutafakari na hatimaye kumwilisha Neno la Mungu
katika huduma makini kwa jirani, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Ni matumaini ya Patriaki Sako kwamba, wananchi wanaoishi huko Iraq na Mashariki
ya Kati, maeneo ambayo kwa sasa yamegeuka kuwa ni uwanja wa vita wataweza kufungua
ukurasa mpya wa maisha, kwa kuwa na amani na utulivu, huku utu na maisha ya binadamu
yakiheshimiwa na kuthaminiwa kwani hii ni zawadi ambayo haina mbadala.
Wananchi
wanaishi katika mazingira hatarishi kiasi kwamba, hawana uhakika wa usalama wa maisha
yao. Familia nyingi zimesambaratika na kutawanyika sehemu mbali mbali, utadhani ni
umande wa asubuhi na kwamba, kuna idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wasiokuwa
na mahali pa kujisetiri.
Licha ya magumu haya yote, lakini Patriaki Sako anawaalika
waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutokata tamaa, bali taratibu kuanza
mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa udugu na ushirikiano, kwa kuheshimiana ili kujenga
misingi ya haki na amani; kipaumbele cha kwanza kiwe ni umoja, msamaha na uptanisho
wa kitaifa; tayari kusimamia mafao ya wengi.
Kipindi cha Kwaresima, iwe ni
fursa kwa Wakristo kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho na kimaadili kwa
kukazia: ukweli, uwazi na uaminifu; waamini wajitahidi kujenga upendo na mshikamano
na wote wanaoteseka na kupondeka moyo kutokana na hali ngumu ya maisha. Wakristo watambue
kwamba, wanayo dhamana na utume huko Mashariki ya Kati na kwamba, uwepo wao ni ushuhuda
wa matumaini kwa wale waliokata tamaa; imani kwa wale waliokengeuka; mapendo kwa wale
wasiothamini wala kuwajali ndugu zao kutokana na tofauti za kiimani. Hakuna haja ya
kutaka kufa wala kupondeka moyo, bali kuendelea kuwa na matumaini kwa kesho iliyo
bora zaidi, kadiri ya mpango wa Mungu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.