2015-02-18 11:40:44

Jumatano ya Majivu!


Ibada ya Jumatano ya Majivu, inawaingiza Wakristo katika Kipindi cha Kwaresima, hija ya siku arobaini inayowachangamotisha waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu na jirani. Ni wakati uliokubalika kwa waamini kumfungulia Mwenyezi Mungu na jirani zao, mioyo ya upendo na huruma. Binadamu kwa kupakwa majivu, anakumbushwa kwamba, yeye ni kiumbe cha Mungu aliyeteolewa kutoka mavumbini na mavumbini atarudi tena! Hapa Mwenyezi Mungu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na pili ni kumheshimu binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano ya Majivu mwaka 2014, kwa kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema: kutubu, kujitakasa na kumwongokea Mungu katika safari ya maisha yao ya kla siku, tayari kuadhimisha Fumbo la Pasaka, ili kumshangilia Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Hii ni hija ambayo inajikita katika sadaka, majitoleo pamoja na kuubeba Msalaba.

Baba Mtakatifu anasema, hija ya Kipindi cha Kwaresima inajikita katika mambo makuu yafuatayo: Sala, kufunga na tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma. Mwamini anaalikwa kudhibiti vilema na udhaifu wake, kwa kuchuchumilia neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya mazoezi ya maisha ya kiroho.

Ikumbukwe kwamba, sala ni majadiliano kati ya Mungu na mwamini, ni nguvu imara inayomuunganisha mwamini na Muumba wake, kwa kutambua udhaifu na mapungufu yake, kiasi cha kukimbilia huruma na upendo wa Mungu. Kwaresima ni kipindi cha Sala inayomwilishwa katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ni muda wa kufunga na kujinyima na wala si kulimbikiza kile ulichojinyima, bali hii ni sehemu ya mkakati wa mabadiliko ya ndani, unaotaka kumsaidia mwamini kuwa na moyo pamoja na huruma kama ya yule Msamaria mwema, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Hapa waamini wanahamasishwa kuwa na kiasi na kujinyima kwa ajili ya wengine. Kwaresima ni kipindi cha kutoa sadaka, kwani inapendeza kutoa kuliko kupokea, waamini wajifunze kutoa kwa ukarimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.