2015-02-17 09:48:41

Washeni taa ya imani!


Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, Jumatatu jioni, tarehe 16 Februari 2015 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa ajili ya kumwombea na kumsindikiza Marehemu Kardinali Karl Josef Becker, S.J. aliyefariki dunia hivi karibuni. Hata katika majonzi na simanzi ni siku ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, aliyemwita Kardinali Becker kumfuasa Kristo katika maisha ya Ukuhani na sasa amemwita kwake, ili kumshirikisha huruma yake.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya adhimisho la Misa Takatifu, alihitimisha kwa Ibada ya Maziko kwa ajili ya Kardinali Becker, kielelezo cha mshikamano wa umoja na mapendo hadi dakika ya mwisho, pamoja na kuendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa kazi kubwa iliyofanywa na Marehemu Kardinali Becker katika kufundisha na kuwafunda vijana wa kizazi kipya, lakini zaidi kwa ajili ya kuwanoa Wakleri katika maisha na utume wao. Marehemu Kardinali Becker alijitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Kiulimwengu.

Kardinali Sodano katika mahubiri yake anasema, kwa wale waliobahatika kumfahamu Marehemu Kardinali Becker wataendelea kumkumbuka kwa kuwa kweli ni jaalim la hekima ya Kikristo, aliyoifundisha kiasi kwamba iliangaza akili na kuupasha joto moyo wa mwanadamu, ili kufungua malango ya maisha kwa Kristo, Mwalimu na Bwana. Ni kiongozi aliyewafunda watu mambo na upendo wa Kimungu, ili kuweza kujiandaa barabara kukutana na Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo.

Kardinali Sodano anaendelea kusema kwamba, huu ndio ukweli wa imani kwa mtu anayeamini, imani ambayo imedhihirishwa na Marehemu Kardinali Becker katika mafundisho yake, alipokuwa anawashirikisha wanafunzi wake imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na imani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu; sasa Marehemu Kardinali Becker anamwona Mwenyezi Mungu uso kwa uso kama ilivyokuwa hamu ya moyo wake.

Kardinali Sodano anawataka waamini kukesha na kuwa macho, kwa kuhakikisha kwamba, taa za maisha yao ya kiroho daima zina mafuta ya kutosha, tayari kumpokea Bwana arusi anapokuja. Hii ni taa ya imani ambayo daima haina budi kuwa inawaaka bila kuzimika. Marehemu Kardinali Becker ni mfano wa kuigwa kwani anasema, onjeni na mwone jinsi Bwana alivyo mwema na heri yake mtu yule anayemkimbilia Bwana ili kutafuta hifadhi kwake.

Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa Makardinali ambao wengi wao walikuwa bado wako mjini Vatican baada ya kuhitimisha mkutano wa Makardinali pamoja na kuwasimika Makardinali wapya ishirini waliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.