2015-02-17 11:22:54

Sauti ya wanyonge!


Kardinali Berhaneyesus Derew Souraphiel, ni kati ya Makardinali wapya 20 waliosimikwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 14 Februari 2015 katika Ibada iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kutoka Barani Afrika, Kanisa limewapata Makardinali wapya watatu, jambo la kumshukuru Mungu. RealAudioMP3
Kardinali Souraphiel anasema, Kanisa bado linawajibu wa kuwa ni sauti ya wanyonge, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu. Kanisa ni sauti ya kinabii kwa wale wasiokuwa na sauti, ni mtetezi wa wanyonge, kwani Kanisa ni sauti ya kimaadili. Sauti ya Familia ya Mungu Barani Afrika inapaswa kusikika, kwani kuna watu wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na umaskini, ujinga na maradhi wakati ambapo kuna raslimali nyingi ambazo zingeweza kuiendeleza Familia ya Mungu Barani Afrika.
Kardinali Souraphiel anapongeza changamoto zinazoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa hususan katika mabadiliko ya Sekretarieti kuu ya Vatican, mada ambayo imejadiliwa na Makardinali katika mkutano wao wa siku mbili hapa mjini Vatican. Anasema, Baba Mtakatifu anapenda kukazia dhana ya Kanisa la Kiulimwengu, kwa kuwa na wawakilishi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kujenga Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Makardinali wapya 20 kutoka katika nchi 18 wanaonesha mwelekeo wa mabadiliko makubwa yanayoendelea kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.
Ikumbukwe kwamba, Makardinali ndio washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika utekelezaji wa dhamana na utume wake kwa Kanisa la Kristo na kwamba, hiki si cheo cha heshima. Makardinali wataendelea kumsaidia Baba Mtakatifu kwa kuchangia kadiri ya uwezo wao, ustawi na maendeleo ya Kanisa. Hapa Kanisa halina budi kujipambanua anasema Kardinali Souraphiel kwa kuwa ni sauti ya wanyonge na maskini, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea utu na heshima ya binadamu, ustawi na mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu Francisko anataka kuliona Kanisa maskini kwa ajili ya huduma kwa maskini; Kanisa ambalo daima linafanya hija ya maisha na watu wakati wa raha na shida, wakati furaha na shangwe. Hapa mtu na utu wake wanapewa kipaumbele cha kwanza kuliko mambo mengine yote. Anakazia mshikamano wa upendo na udugu; majadiliano ya kidini na kiekumene. Ni kiongozi anayependa kuwatetea wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Papa Francisko amekuwa ni msemaji mkuu na mtetezi wa wahamiaji kutoka Barani Afrika wanaoendelea kufariki dunia huko kwenye Bahari ya Mediterrania, wakiwa na matumaini ya kufika Ulaya, ili waweze kuboresha maisha yao, lakini ndoto zote hizi zinapotelea katika tumbo la Bahari ya Mediterrania kama yalivyo machozi ya samaki yanaishia majini. Kuna haja ya kupambana kufa na kupona na wafanyabiashara haramu wa binadamu, ili kukomesha utumwa ambao unaendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu.
Bara la Afrika halina budi kuwekeza katika elimu, ili kuwakomboa wananchi wengi kutoka katika lindi la ujinga na maradhi. Kuwepo na mikakati na sera nzuri zitakazozalisha ajira kwa vijana, ili waweze kuondokana na ndoto ya mchana kwamba, maisha mazuri yanapatika Ulaya! Elimu inaweza kuwasaidia vijana kuboresha maisha yao hatua kwa hatua.
Ni matumaini ya Kardinali Souraphiel kwamba, iko siku, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ataweza kutembelea Ethiopia na hatimaye, kupata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa Umoja wa Afrika. Baba Mtakatifu anaendelea kukazia kwamba, uongozi ni huduma na wala si ujiko!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, kwa msaada wa NCR.








All the contents on this site are copyrighted ©.