2015-02-17 11:01:59

Nimekosa!


Kabla ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mama Kanisa ametuwekea utaratibu wa kuchunguza dhamiri zetu, ili kuomba toba na msamaha wa dhambi na hatimaye kuadhimisha mafumbo ya Kanisa kwa ibada na uchaji mkuu. Ebu chukua muda kidogo ufanye tafakari kuhusu sala hii katika maisha yako ya kila siku!
"Namuungamia Mungu Mwenyezi, nanyi ndugu zangu kwani nimekosa mno; kwa mawazo, kwa maneno, kwa matendo na kwa kutokutimiza wajibu. Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa mno. Ndiyo maana namwomba Bikira Maria mwenye heri, Mama wa Mungu, Malaika na Watakatifu wote, NANYI NDUGU ZANGU niombeeni kwa Bwana Mungu wetu"
Sala hii huwa tunaisali karibu kila siku, na kila tushirikipo Ibada ya Misa Takatifu. Ni sala ambayo tumeizoea sana katika maisha yetu ya kila siku. Leo kwa namna ya pekee tuirudie sala hii na kisha tutafakari baadhi ya vipengele vyake hasa nafasi ya ndugu katika maisha yetu ya kawaida ya kila siku na yale ya utakatifu.
Ndugu zetu, hasa, wazazi wetu, wenza wetu wa ndoa, wanafamilia, ndugu wa mbali na wa karibu, jamaa zetu, marafiki, wafanyakazi wenzetu n.k Je, wana nafasi gani katika maisha yetu? Tunaitambua nafasi yao muhimu katika maisha yetu? Tunawatendea haki na kuiheshimu nafasi yao?

Mara nyingi hatufahamu nafasi yao na hivyo huwa tunawakosea sana; tunawatukana, tunawakasirisha, tunawasengenya, tunawahukumu, tunawashudia uongo, tuwadhulumu, tunawatapeli, tunawaomba rushwa, tunawazulia mabaya na kuwaombea yawapate mabaya, tunawaharibia, kuwaficha na kuwazibia fursa zao za maendeleo. Hatutumizi wajibu zetu kwao kama wazazi, wakubwa, wazee wa jamii, kama watoto, viongozi na kuliko yote kama wakristu.
Wajibu hizi ni pamoja na kuwashauri, kuwakosoa, kuwakemea, kuwapa mahitaji ya kila siku, kuwaongoza vyema ili kitimiza wajibu zao na kutenda mema, kuwapenda.
Hao ndugu zetu wana nafasi kubwa sana katika maisha yetu km nilivyosema hapo juu. Wana nafasi ya kuturekebisha, kutuombea, kutusaidia ktk mambo mbalimbali, wa kutuonesha na kuuona ukuu wa Mungu kwao. Hao ndiyo tunaoishi nao kila siku, wanatufahamu vizuri sana. Vitabu vinatuambia kuwa hatuwezi kusema kuwa tunampenda Mungu ambaye hatumuoni wakti tunamchukia mwanadamu mwenzetu tunayeishi naye kila siku. Kwa kumpenda na kumjali mwanadamu mwenzetu tutakuwa tunampenda Mungu na lolote tunalomtendea mwanadamu mwenzetu tunamtendea Mungu.
Wapendwa, tunaingia katika kipindi cha Kwaresma, kipindi cha toba, ni wakati wa kutafakari utajiri na tunu iliyofichika katika ndugu zetu, tujichunguze na kuona kwa kiasi gani tulikosa, tumekosa na tunaendelea kukosa kwao. Sala hii itutafakarishe nafasi ya ndugu zetu katika ukombozi wetu.
Ni kipindi cha kutubu, kuombana msamaha na kusameheana. Tukitumie kipindi hiki cha Kwaresma tunachokianza kwa kupakwa majivu, alama ya toba ili kurudisha mahusiano mema katika familia zetu, makazini, kwenye Jumuiya, makanisani na katika jamii kwa ujumla. Tuache kiburi na kisirani na kujiona sisi ni watenda haki zaidi kuliko wenzetu, tuwe wepesi wa kutenga muda wa kutafakari maisha yetu na nafasi ya ndugu zetu katika maendeleo na katika wokovu wetu.
Tushiriki kiaminifu matukio mbalimbali katika kipindi hiki. Hayo ni pamoja na Jumatano ya Majivu ambayo ni siku ya kufunga chakula, njia ya msalaba kila Ijumaa, tafakari za mateso, semina za kukua kiroho, matendo ya huruma kwa kuwajali ndugu zetu wahitaji na kuwapelekea kile tulichojinyima katika kipindi hiki. Tuhitimishe na Juma kuu la mateso.
Tujiepushe na matendo maovu na starehe za kidunia. Mwisho wa kipindi hicho cha Kwaresma, tujifanyie tathmini kama tumebadilika kiasi gani. Nawatakieni wote mwanzo mwema wa kipindi cha Mfungo na Toba.
Tumsifu Yesu Kristo !
Na Antipasi Shinyambala
Jimbo kuu la Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.