2015-02-17 09:54:07

Kilio cha damu!


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na taarifa ya mauaji ya kinyama yaliyofanywa dhidi ya Wakristo wa Kanisa la Kikoptik la Misri waliokuwa wametekwa nyara huko Sirte, nchini Libya. Hawa wameuwawa na Wanajeshi wa Jihadi kwa vile tu walikuwa ni waamini wa dini ya Kikristo.

Hii ni chuki ya imani isiyokuwa na mashiko katika kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu. Hii ni damu ya watu wasiokuwa na hatia ambayo inaendelea kusikika sehemu mbali mbali za dunia, watu wanaonyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anasema, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni, tarehe 16 Februari 2015 amepiga simu na kuzungumza na Patriaki Papa Tawadros wa Pili, ili kumshirikisha masikitiko yake na kumwonesha mshikamano wa kidugu katika kipindi hiki cha majonzi. Baba Mtakatifu anasikitishwa na mauaji ya kinyama yaliyofanywa na waamini wa dini ya Kiislam wenye msimamo mkali wa kidini. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wahanga na wote walioguswa na msiba huu mkubwa, uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala.

Baba Mtakatifu, Jumanne, tarehe 17 Februari 2015 katika Ibada ya Misa takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican amewakumbuka na kuwaombea Wakristo waliouwawa kikatili kutokana na chuki za kidini, ili waweze kupata furaha ya uzima wa milele, wa yule ambaye wamemwaminia katika maisha yao kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.