2015-02-17 11:18:34

Jikiteni katika maadili ili kukuza uchumi!


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, mchakato wa maendeleo na maboresho katika sekta ya uchumi unakwenda sanjari na kanuni msingi za maadili na utu wema, mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya kiuchumi, vinginevyo, mkwamo wa uchumi utaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu sehemu mbali mbali za dunia.
Ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Kardinali Oscar Andrès Rodrigues Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, wakati wa kuzindua kitabu kilichoandikwa na Bwana Andrea Tornielli kuhusu mchakato wa ukuaji wa uchumi kadiri ya mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko.
Kuna haja ya kuwa na ujasiri wa kubadili sera na mfumo wa uchumi ikiwa kama hautowi kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, utu na heshima yake. Tabia ya kujinyima kwa ajili ya mafao ya maisha ya kiroho na kimwili ni fadhila ya Kikristo, lakini kuwalazimisha watu kufunga mikanda kiasi cha kuwatesa baadhi ya wananchi kwa kuwasukumiza pembezoni mwa jamii, wakati wengine wakiendelea kula kuku kwa mrija si jambo la haki na wala halipendezi machoni pa Mungu. Sera za uchumi wa namna hii ni mauaji kwa watu wasiokuwa na hatia.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji Injili ya Furaha anafafanua kwa kina na mapana umuhimu wa sera na mikakati makini ya kiuchumi inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, utu na heshima yake. Mkazo ni kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata huduma msingi katika sekta ya elimu, afya na maendeleo.
Wananchi wapate fursa za ajira ili kuzitegemeza familia zao, sanjari na kuendeleza mchakato wa upendo na mshikamano kati ya watu unaoongozwa na kanuni auni; mambo msingi kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa; ambayo wataalam wengi wa uchumi wanayasahau, lakini ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya binadamu wote, kwani hapa kipaumbele cha kwanza ni binadamu na mafao ya wengi.
Bwana Andrea Tornielli mwandishi wa kitabu hiki anasema, lengo ni kuwachangamotisha wataalam na watunga sera za uchumi na maendeleo kufungua macho, ili kuona pia mchango wa Mafundisho Jamii ya Kanisa katika ustawi na maendeleo ya binadamu badala ya kuendelea kujikita katika sera za uchumi ambazo zimejielekeza zaidi katika taasisi za fedha ili kutafuta faida kubwa na matokeo yake ni athari za myumbo wa uchumi kimataifa, jambo ambalo kwa sasa ni janga la watu wengi, kwani ukuaji wa uchumi unaendelea kusua sua licha ya sera na mikakati iliyobainishwa na kupangwa na wachumi waliobobea katika fani hii.
Mshikamano wa upendo ni dhana ambayo pia haina budi kumwilishwa katika uhalisia wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu, kwani hili ni jambo linalowezekana kabisa na wala hapa si kutetea wala kulinda siasa ya kikomunisti, kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyobainisha katika mahojiano maalum na mwandishi wa kitabu hiki, kwani upendo na mshikamano ni tunu ambazo hazina mipaka wala vizingiti.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.