2015-02-17 09:57:03

Hatoki mtu hapa!


Askofu Giovanni Innocenzo Martinelli, mwangalizi wa kitume wa Jimbo la Tripoli, Libya ambaye kwa miaka zaidi ya arobaini amekuwa akiishi na kutekeleza utume wake nchini Libya anasema, hata katika hali tete kiasi hiki ambako maisha ya wananchi wengi wa Libya yako hatarini, ataendelea kubaki nchini Libya hadi kieleweke!

Anasema ataendelea kubaki na kushikamana nao, tayari kushuhudia imani yake kwa Kristo na Kanisa lake, hata kama itambidi kutoa sadaka ya maisha yake. Lengo ni kuwatia shime pamoja na kuendelea kuwahudumia wagonjwa na majeruhi, kazi inayofanywa na watu wa kujitolea wanaosimamiwa na Kanisa mahalia, wengi wao ni wahamiaji kutoka Barani Asia.

Kamwe hataogopa kuendelea kushikamana na Wakristo ambao kwa sasa wanatishiwa maisha na wanajeshi wenye misimamo mikali ya kiimani wanaoendelea kuvuruga Libya. Wanajeshi wa Jihadi tayari wamekwisha tua nanga mjini Tripoli, changamoto ya kusimama kidete katika misingi ya imani, tayari kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kina kwa njia ya ushuhuda wa maisha bila ya kukata tamaa, ili kujenga utamaduni wa kuwapenda na kuwathamini wengine, tayari kushirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Vita hii inayoendelea kutikisa ulimwengu anasema Askofu Martinelli, nyuma yake kuna sababu za kiuchumi, wajanja wanataka kuchukua mafuta kutoka Libya pamoja na kuendelea kufanya biashara haramu ya silaha na binadamu; jambo ambalo kwa sasa lina faida kubwa kwa watu ambao dhamiri zao zimekufa. Kuna haja ya kuwa na ujasiri wa kushutumu njama hizi pamoja na kuanza mchakato wa majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi, ili hatimaye, kujenga utamduni wa udugu na mshikamano.

Hii ni changamoto kubwa kwa Nchi za Falme za Kiarabu na Jumuiya ya Kiislam, kusaidia mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani kati ya watu kwani vita haina macho wala pazia. Watu wengi wanajiuliza, Je, ni nani ambaye anawakingia kifua hawa wanajeshi wa Jihadi, ni nani anayewapatia fedha kiasi cha kuwa na jeuri ya kuua watu bila hata chembe ya huruma? Bila shaka anasema Askofu Martinelli, hii ni fedha ya damu kutoka katika visima vya mafuta huko Mashariki ya Kati.

Wakristo wahamiaji wanaoishi nchini Libya hata katika ukimya wao wanaendelea kushuhudia imani katika matendo, kwa kuwaonjesha huruma na mapendo, wale wote wanaoteseka kutokana na vita na kinzani za kijamii. Askofu Martinelli anatambua fika changamoto kubwa iliyoko mbele yake na kwamba, maisha yake yako hatarini, lakini kama Mchungaji mwema anaendeleo kuonesha ujasiri, moyo mkuu na mshikamano na wale wanaoteseka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.