2015-02-17 12:21:44

Biashara ya silaha ni chanzo cha majanga kwa mataifa!


Katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Kikanisa Cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumanne tarehe 17 Februari 2015, Baba Mtakatifu Francisko ametolea nia ya Ibada hii ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo waliouwawa kikatili nchini Libya.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anasema kwamba, kila mtu ana uwezo wa kutenda mema na kuachana na mabaya. Binadamu anaweza kugeuka na kuwa mkatili kiasi hata cha kuvuruga mahusiano na udugu kati ya watu; hili ndilo chimbuko la vita na kinzani mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia. Baba Mtakatifu anawashutumu wafanyabiashara wanaoendelea kuuza silaha kwenye maeneo ya vita, ili kuchuma faida kubwa kwa gharama ya maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

Baba Mtakatifu anasema, binadamu ana uwezo wa kuharibu kazi ya uumbaji ambayo amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu kuilinda, kuitunza na kuiendeleza kwa ajili ya mafao ya sasa na yale ya kizazi kijacho. Ni kutokana na kiburi na majivuno ya mwanadamu, mauti imeingia duniani kama ambavyo Liturujia ya Neno la Mungu ilivyoonesha. Mwanadamu anataka kujikweza na kudhani kwamba, anaweza kuwa ni sawa na Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, Sura kadhaa kutoka katika Kitabu cha Mwanzo zinaonesha udhalimu na dhambi inavyojikita katika moyo wa mwanadamu, kiasi hata cha Kaini kumwangamiza ndugu yake Abeli kutokana na wivu usiokuwa na mashiko, hapa ukawa ni mwanzo wa chuki, uhasama na vita kati ya watu. Baba Mtakatifu anasema kwamba, leo hii asilimia kubwa ya habari zinazotawala katika vyombo vya habari ni kuhusiana na majanga ya: vita, mauaji na kinzani za kijamii. Hapa Baba Mtakatifu anajiuliza ni jambo gani ambalo haliendi sawa katika moyo wa mwanadamu?

Hapa Mwenyezi Mungu anapenda kumwonesha mwanadamu kwamba, moyo wake umejeruhiwa vibaya sana, kiasi cha mwanadamu kujitafutia uhuru usiokuwa na mipaka hata kama ni kwa ajili ya maangamizi yake! Biashara ya silaha ni kati ya mambo yanayochochea vita na kinzani za kijamii, kiasi hata cha kupandikiza mbegu ya kifo ili kujipatia faida kubwa inayotokana na damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuchagua kutenda mema na kuachana na maovu; kuachana na wivu, masengenyo na uchoyo usiokuwa na mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu. Hali hii imejitokeza hata miongoni mwa mitume wa Yesu, wakaanza kusigana kwa vile walisahau kuchukua mkate!

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuachana na chachu ya Mafarisayo ambao ni wanafiki na Herode ambaye ni katili na muuaji na badala yake watambue kwamba, wokovu ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wajitahidi kuchagua na kutenda mema kama alivyofanya Mama Theresa wa Calcutta kwa kujisadaka kwa ajili ya maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Wazazi na walezi wawasaidie watoto wao kukua katika fadhila na utu wema bila kusahau kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu ili awaepushe na mitego ya Shetani.

Yesu Kristo anawakumbusha wafuasi wake kwamba, amemwaga Damu yake Azizi kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kumkirimia mwanadamu uweo na nguvu ya kutembea katika mwanga mpya wa maisha kwa njia ya majadiliano katika maisha ya kifamilia, kijamii na kitamaduni, ili kujenga na kukuza utamaduni wa upendo na mshikamano.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, Kipindi cha Kwaresima kinachoanza kwa kupakwa na majivu ni muda wa neema na baraka, kamwe wasimwachie nafasi Shetani ili aweze kuwalaghai na kuwapeleka kwenye njia ya upotofu. Waamini wawe imara na thabiti katika maisha yao ya kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.