Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 16 Februari 2015 amekutana na kuzungumza
na ujumbe wa Kanisa la Scotland uliomtembelea mjini Vatican kwa kuendelea kukazia
umuhimu wa Wakristo kujikita katika Injili pamoja na kuendeleza umoja wa Wakristo,
kwa kutambua kwamba, Scotland ni nchi ambayo ina utajiri mkubwa wa kitamaduni na kihistoria,
kwa kuwa na watakatifu pamoja na mashuhuda wengi wa Kikristo.
Hali ya mchakato
wa majadiliano ya kiekumene nchini Scotland inaonesha kwamba, kuna mambo mengi ambayo
yanawaunganisha Wakristo kuliko hata yale yanayowagawa na kuwatenganisha, changamoto
kwa Wakristo kuvuka kikwazo cha kudhaniana vibaya na kuanza kutafuta njia mpya za
maelewano na ushirikiano, ili kwa pamoja kuweza kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa
katika ulimwengu mamboleo; kwa kuwa na sauti moja kwa mambo yale yanayowagusa kama
Wakristo.
Katika ulimwengu wa utandawazi ambamo unaonekana kuchanganyikiwa,
kuna haja kwa Wakristo kuonesha ushuhuda wa pamoja kama kikolezo cha uinjilishaji
makini kwa kutambua kwamba, wote wanafanya hija ya pamoja, changamoto kubwa ni kuaminiana
ili kwa pamoja kama mahujaji waweze kuutafuta uso wa Kristo. Imani na ushuhuda wa
Kikristo vinakabiliwa na changamoto nyingi kiasi kwamba, umoja na mshikamano ndiyo
njia pekee itakayowawezesha Wakristo kuihudumia vyema Familia ya Mungu sanjari na
kumwezesha Kristo kuwafikia watu wengi zaidi.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu
kwamba, hija ya upatanisho na amani kati ya Makanisa haya mawili itawasaidia kuyaunganisha
na kuyaweka kwa pamoja, ili kumwezesha Roho Mtakatifu kuwasaidia kuwapatia watu wengi
maisha na kuzaa matunda mengi. Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe hawa kuendelea kusindikizana
katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya sala.
Na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.