2015-02-16 15:07:24

Shukrani kwa kupata Kardinali!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 16 Februari 2015 amekutana na kuzungumza na Mfalme Tupou wa VI na mke wake, kutoka Visiwa vya Tonga ambaye baadaye walikutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Mfalme Tupou VI amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kumteua Kardinali Soane Patita Paini Mafi kutoka Kisiwa cha Tonga na kwamba, wananchi na watu wote wenye mapenzi mema wameungana na Makardinali wote kuonesha furaha yao Jumamosi, tarehe 14 Februari 2015 wakati Makardinali wapya walipokuwa wanasimikwa rasmi.

Viongozi hawa wawili katika mazungumzo yao wameendelea kujielekeza katika masuala ya maendeleo ya kisiasa yaliyojitokeza nchini humo hivi karibuni mintarafu uchumi na maisha ya kijamii pamoja na mchango endelevu unaotolewa na Kanisa Katoliki nchini humo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Wamebadilishana mawazo kuhusiana na masuala ya kimataifa, huku wakirejea kwenye Visiwa vya Pasific pamoja na matatizo ya uchafuzi wa mazingira yanayojitokeza katika eneo hili; changamoto ambayo haina budi kufanyiwa kazi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.