2015-02-16 09:24:20

Sensa ya Viwanda Tanzania kutimua vumbi 23 Februari 2015


Serikali ya Tanzania imesema kuwa maandalizi ya Sensa ya Viwanda ya mwaka 2013 itakayofanyika nchi nzima kuanzia Februari 23 mwaka huu yamekamilika hivyo wamiliki wa viwanda na wadau mbalimbali wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakaopita katika maeneo yao kukusanya takwimu wakati wa Sensa hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo na kuwaapisha wasimamizi na wadadisi wa Sensa ya Viwanda ya mwaka 2013 iliyofanyika katika Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika jana jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa alisema kuwa maandalizi ya awali ya Sensa hiyo yamekamilika yakihusisha uhamasishaji wa ushiriki wa wenye viwanda kwenye Sensa hiyo, utoaji wa elimu kwa wadadisi na wasimamizi watakaoendesha zoezi hilo.

Alisema kuwa kutokana na umuhimu wa Sensa hiyo wamiliki wa viwanda katika maeneo mbalimbali watashiriki kutoa takwimu zitakazojazwa katika madodoso maalum yaliyoandaliwa ili kuliwezesha taifa kuweka Sera na mipango ya maendeleo inayotokana na takwimu sahihi za viwanda vilivyopo nchini. Aliongeza kuwa mafanikio ya Sensa hiyo yatatokana na wamiliki wa viwanda kutambua na kuithamini Sensa hiyo kwa kutoa ushirikiano wa kuwapatia takwimu sahihi wadadisi watakaopita katika maeneo yao kukusanya taarifa zinazohusu masuala mbalimbali yakiwemo ya uzalishaji wa bidhaa na masuala ya ajira; Dkt. Chuwa alibainisha kuwa upatikanaji wa takwimu sahihi kuhusu Sekta ya Viwanda nchini Tanzania utaiwezesha Serikali kutambua mchango wa viwanda katika ajira, uzalishaji na pato la taifa hivyo kuweka Sera na mipango endelevu ya maendeleo itakayoliwezesha taifa na sekta hiyo kupiga hatua kimaendeleo.

“Sensa hii ya viwanda ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, na mafanikio yake yatatokana na wenye viwanda kutupa ushirikiano maana bila wao kutoa takwimu sahihi mipango ya maendeleo kuhusu viwanda haitatekelezeka kwa sababu ya kukosa takwimu sahihi” Amesisitiza Dkt. Chuwa. Kuhusu wasimamizi na wadadisi watakaoendesha zoezi hilo litakalofanyika kwa muda wa miezi 3, Dkt. Chuwa aliwataka wafuate sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu bora.

Naye Mkurugenzi wa shughuli za Takwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Aldegunda Komba akizungumza na wadadisi hao alisema kuwa wadadisi hao wamepewa dhamana kubwa ya kutimiza lengo liliowekwa na Serikali la kuwa na takwimu sahihi kuhusu mchango wa viwanda katika maendeleo ya taifa. “Mafunzo tuliyowapatia kwa vitendo na nadharia yamewajengea uwezo wa kukusanya takwimu bora, tunaomba zoezi hili mlifanye vizuri tunatarajia mtaitumia vizuri elimu mliyoipata kwa kufanya kazi kwa umakini mkubwa kwa manufaa ya taifa letu”. Amesisitiza Bi. Komba.

Aidha, alibainisha kuwa kukamilika kwa Sensa hiyo kutaliwezesha taifa kutambaua mchango wa Sekta ya Viwanda katika uchumi na pato la taifa. Kwa upande wake Kamishna wa Viapo ambaye pia ni Mwanasheria wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Oscar Mangula akizungumza na wasimamizi na wadadisi wa Sensa hiyo aliwataka kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia zoezi hilo.








All the contents on this site are copyrighted ©.