2015-02-16 14:47:52

Jifunzeni kutoka kwa maskini!


Hija ya maisha ya kiroho inayotekelezwa na wanachama wa Mfuko kwa ajili ya Kiti cha Mtakatifu Petro ni kielelezo cha uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kuna ongezeko kubwa la maskini wa maisha ya kiroho na kimwili na kwa upande mwingine,watu wanaweza kujichotea utajiri mkubwa kutoka kwa maskini, wanaowasogelea na kuwahudumia kwa upendo.

Hili ni kundi ambalo licha ya ugumu na umaskini wake, linaendelea kulinda na kutunza tunu msingi za maisha ya kifamilia, ni watu wenye uwezo mkubwa wa kugawana kile kidogo walicho nacho na maskini zaidi; kwa hakika ni watu ambao wanafuraha inayobubujika kutokana na uhalisia wa maisha yao, hali ambayo amejionea mwenyewe anasema Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Barani Asia.

Hii ni hotuba ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa kusaidia Kiti cha Mtakatifu Petro, walipomtembelea mjini Vatican, siku ya Jumatatu tarehe 16 Februari 2015. Hali ya kutowajali wengine pamoja na ubinafsi inahatarisha maisha ya wengi, lakini huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni jambo ambalo linawatajirisha wengi kwa kuwaonesha njia ya unyenyekevu na ukweli. Uwepo wao ni utajiri mkubwa katika ubinadamu, kwa kutambua udhaifu wa maisha na hali ya kumtegemea Mwenyezi Mungu na jirani.

Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe hawa kwa namna ya pekee kabisa wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya kukianza Kipindi cha Kwaresima, kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia moyo wa huruma na umaskini, unaotambua umaskini wake, ili kujisadaka na kujitoa kwa ajili ya wengine.

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza wajumbe hawa kwa mchango wao, utakaosaidia kutoa huduma kwa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha. Ni kielelezo cha mshikamano unaoleta faraja moyoni, kiasi cha watu kujisikia kwamba, hata katika shida na magumu ya maisha, bado kuna watu wanaowakumbuka na kuwathamini, hivyo wanapaswa kuendelea kuwa na matumaini pasi na kukata tamaa.

Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe hawa kusali zaidi kwa ajili ya kuombea amani duniani, ili viongozi wa kisiasa waweze kujikita katika njia ya majadiliano na upatanisho. Anawatakia kheri na baraka tele, ili waweze kutambua kwamba, hija wanayoitekeleza kwenye Makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume iwasaidie kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya Kanisa, Familia kubwa na watu ambao wanafuraha ya kutangaza Injili kwa watu wote.

Waendelee kujenga na kudumisha udugu kati yao, ili kutekeleza huduma kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watu ambao walipewa upendeleo wa pekee na Yesu katika maisha na utume wake. Mwishoni, kabisa, Baba Mtakatifu amewaweka wajumbe hawa chini ya ulinzi, tunza na maombezi ya Bikira Maria, Mtakatifu Petro na Watakatifu wasimamizi wa nchi zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.