Baraza la Maaskofu Katoliki Poland katika barua yake ya kichungaji kama sehemu ya
maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, linakazia umuhimu wa mshikamano kati ya familia
na maisha ya kitawa, kwa kutambua kwamba, familia ni chimbuko la miito mitakatifu
na mahali pa kukuza na kulelea miito hii.
Katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia wanasema Maaskofu, watu wengi
wanamezwa mno na malimwengu, ubinafsi na uchoyo; kinzani na migawanyiko. Watawa ni
mashuhuda wa maisha ya Kijumuiya na kielelezo kwamba, maisha upendo na udugu si kikwazo
katika ukuaji wa mtu: kiroho na kimwili, bali ni chachu ya mshikamano wa upendo dhidi
ya ubinafsi na kinzani.
Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linabainisha kwamba,
kuna uhusiano mkubwa kati ya Familia na Maisha ya Kitawa; kuna tofauti kubwa inayojionesha
katika karama za Mashirika ya kitawa na kazi za kitume, zote hizi ni kazi ya Roho
Mtakatifu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa; karama hizi zinakamilishana
na wala hakuna misigano.
Ni wajibu wa familia za Kikristo kuendelea kuboresha
maisha na utume wao, kwa kuiga mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu,
bila kusahau umoja unaojikita katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baraza la Maaskofu
Katoliki Poland linahitimisha barua yake ya kichungaji kwa Familia ya Mungu nchini
humo kwa kukumbusha kwamba, familia za Kikristo ni chemchemi ya miito mitakatifu ndani
ya Kanisa; hapa ni mahali pa watu kujifunza, ubaba, umama na udugu kama msingi wa
imani katika mchakato wa maisha ya kitawa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.