Mpendwa msikilizaji wa Kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, tumsifu Yesu Kristo,
Laudetur Iesus Christus! Kwa mara nyingine tena tuendele kuzichambua hati za Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican, ambamo Mama Kanisa anatufundisha mambo mbalimbali yenye kutujenga
katika Ukristo wetu.
Katika vipindi
vilivyopita, baada ya kuyatupia macho matamko yale mawili yaani Gravissimum educationis
(tamko lililohusu uzito wa malezi) na Dignitatis humanae (tamko lililohusu uhuru wa
dini), leo mpendwa msikilizaji tulitegee sikio tamko la tatu linalohusu uhusiano wa
Kanisa na dini zisizo za Kikristo, kwa lugha ya Kilatini tamko hili linaitwa Nostra
Aetate, likimaanisha Wakati Wetu!
Mtaguso Mkuu ulizingatia ukweli kwamba watu
wa wakati wetu wanazidi kuunganishwa kwa namna mbalimbali, na kunaonekana utegemeano
dhahiri kati ya watu wa mataifa mbalimbali ya dunia. Ni kwa ukweli huo, Kanisa nalo
linahimiza tabia ya mahusiano mema na dini zisizo za Kikristo. Linahamasisha umoja
na upendo kati ya wanadamu, kati ya mataifa mbalimbali kwa sababu watu wote ni jumuiya
mmoja, asili yao ni mmoja, na ni Mungu ndiye aliyewaweka wote wakae juu ya uso wa
nchi.
Ndani ya Nostra aetate, yaani Wakati Wetu, Kanisa linazitazama dini mbalimbali
kama ishara ya kiu ya mwanadamu ya kutaka kujua ukweli wa ndani juu ya uumbaji, maisha,
mateso, kifo na maisha baada ya kufa. Katika dini zote, mwanadamu anakiri uwezo fulani
mkuu ambao ni chanzo na kikomo cha yote. Daima mwanadamu huyu hutafuta muungano na
hiyo Nguvu kuu, ambayo kwayo husaidiwa kupata maana ya uhalisia wa maisha ya kila
siku. Pamoja na mambo mengine mengi, katika dini mwanadamu ataka kujua binadamu ni
nini, maana na mwisho wa maisha yake ni nini, dhambi na tendo jema ni nini, chanzo
na lengo la mateso ni nini, njia gani inatupeleka kwenye furaha ya kweli, mauti na
hukumu ni nini. Zaidi pia binadamu ataka kujua, anatoka wapi na anakwenda wapi.
Nostra
aetate, Wakati Wetu, yatuambia; Kanisa Katoliki linaamini ukweli wa Kihistoria kwamba,
tangu zamani za mwanadamu dini mbalimbali zimekuwa ni kielelezo cha hiyo kiu ya mwanadamu,
na hivyo linaheshimu sana mambo yote yaliyo kweli na matakatifu katika dini nyinginezo.
Linaheshimu kwa sifa timamu sheria zote na mafundisho ambayo yana mwanga fulani wa
ukweli wa kuwaangazia watu, hata kama mambo hayo ni kinyume cha yale ambayo Kanisa
lenyewe linasadiki na kufundisha. Pamoja na kuheshimu ukweli huo ulioko katika dini
nyinginezo, Kanisa na waana Kanisa ni lazima kuendelea kumsadiki na kumtangaza Kristo
Yesu aliye njia, ukweli na uzima.
Ndani ya Nostra aetate, Kanisa latuhimiza
kutoa ushuhuda wa imani ya Kikristo kwa busara na mapendo, kwa njia ya majadiliano
na ushirikiano na wafuasi wa dini nyinginezo, na zaidi ya hayo, Mama Kanisa anatuambia
sisi Wakristo, tujibidishe kutambua na kukuza mema ya kiroho na ya kimaadili na tunu
za kijamii na za kitamaduni zinazopatikana kwa ndugu zetu wasio wa-Kristo.
Mpendwa
Msikilizaji, kwa njia ya Nostra aetate, Kanisa linatuhimiza sisi sote kuishi kwa amani,
umoja, upendo na ushirikiano, kama jumuiya mmoja inayounganishwa kwa pendo la Mungu
Baba. Kwa nini leo watu wanaleta mafarakano duniani kwa jina la dini? Mama Kanisa
daima anafundisha na kutuhimiza ‘tutambuane katika tunu zilizomo kwa kila mmoja wetu,
na tuheshimiane katika tofauti zetu. Sote ni watoto wa Baba mmoja, ambaye ni Mungu,
na sote tunajibidisha kumpenda, kumtumikia na kumwendea yeye kwa njia mbalimbali.
Kwa nini tudharauliane? Mpendwa msikilizaji wa Kanisa la nyumbani, neno hili linakujia
sikioni pako kabisa; ‘wewe na mimi, tujitahidi kuwaheshimu wengine katika dini zao.
Pili, tujibidishe kuwaelewa wale ambao hawaamini kili tunachokiamini sisi, ili tuone
tunu za mwanga wa ukweli zinazowaongoza kwa Mungu. Tatu tutawale sana utashi wetu
na midomo yetu, ili wewe au mimi mmoja wetu asiwe msemaji wa dini ya mwenzake. Kila
mtu aisemee na kuifafanua dini yake mwenyewe. Ukishika kipaza sauti na kumfungia mwenzako
spika-mzinga dirishani ili kuikashifu dini yake, hapo utasambaratisha upendo na amani
itawekwa rehani. Daima ikumbukwe, nafsi ya mtu imeunganika kwa fumbo la ajabu
sana na ukweli kuhusu dini. Pale unapoikejeli dini ya mtu, ni kama unakejeli nafsi
yake na mtaala mzima wa maisha yake. Mtu aheshimiwe tu katika imani yake. Iwapo kuna
jambo unahitaji kuelewa katika dini fulani, basi waulize kwa upole wahusika, wakufafanulie.
Na ukishafafanuliwa na ukaona tunu zao hazikusadifu, usiwakashifu wala kuwadharau,
nyamaza kimya uwaheshimu. Ni kwa upole na heshima, tutajenga upendo. Kwako mpendwa
Mkatoli, sauti pole ya Mama Kanisa inatuagiza, kamwe tusiwe chanzo cha chokochoko
za kidini. Imani, matumaini, mapendo, amani, utulivu, heshima na maelewano mema, daima
viwe dira yetu. Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin
Mkorwe OSB