2015-02-15 09:51:17

Msiwapeleke watoto vitani!


Jumuiya ya Kimataifa bado inaendelea kukabiliana na changamoto ya kuhakikisha kwamba, watoto wanalindwa na kutetewa katika utu na heshima yao na kamwe wasipokwe matumaini ya kuwa na leo na kesho iliyo bora zaidi kwa kupelekwa mstari wa mbele ili kupigana kama wanajeshi. Kuna mikataba na Protokali za kimataifa zilizotiwa sahihi na Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, lakini hata leo hii bado kuna watoto ambao wanabebeshwa silaha na hata wakati mwingine wanafungshiwa mabomu ya kujitosa mhanga ili kufanya mauaji.

Hawa ni watoto ambao, maendeleo na makuzi yao yameingia dosari, lakini hakuna haja ya kukata tamaa, bado jamii ikijika katika kanuni maadili na sheria za kimataifa, watoto hawa wanaweza kufunguliwa ukurasa mpya wa maisha na kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi, inayojikita katika amani, utulivu na maendeleo ya wengi.

Askofu Giuseppe Franzelli wa Jimbo Karoliki Lira, Kaskazini mwa Uganda anabainisha kwamba, kuna zaidi ya watoto 250, 000 ambao wameajiriwa kwenye majeshi na wanapelekwa mstari wa mbele kama chambo vitani kama inavyojionesha huko Iraq, Syria, Somalia, Sudan ya Kusini, Afghanstan, Mali na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.

Hawa ni watoto wanaogeuzwa na kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu; watoto wanaotumiwa kufanya biashara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya. Lakini mbaya zaidi ni watoto wanaofundishwa kuwa na ukatili bila hata chembe ya huruma, hawa baadaye wanageuka kuwa ni majambazi wa kutumia silaha; wakifikia hatua hii, amani na utulivu ndani ya jamii viko mashakani.

Askofu Franzelli anasema, Jimboni mwake, ameshuhudia na kuona watoto ambao wametekwa na hatimaye kugeuzwa kuwa ni wapiganaji wa Jeshi la Waasi nchini Uganda; jambo ambalo linawaachia watoto madonda makubwa ya maisha na maadili. Hapa kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa kwa kuwekeza katika elimu na malezi, ili kuwapatia vijana fursa ya kujiendeleza ili kukabiliana vyema na changamoto za maisha. Kanisa nchini Uganda linaendelea kujielekeza katika kuwahudumia na kuwasaidia watoto kwa kuwapatia elimu makini, kama cheche za matumaini kwa siku za usoni.

Jamii inapaswa kuwaona watoto hawa kuwa ni sehemu ya maisha ya jamii na kamwe si mzigo mzito, ili kuwapenda na kuwathamini, vinginevyo wanaweza kugeuka na kuwa watu wakatiliki wasiokuwa na utu wa huruma. Watoto wanaopelekwa vitana kama wapiganaji ni wahanga wa vita, wasaidiwe na kamwe jamii isiwageuzie kisogo na kuwatelekeza. Kuna baadhi ya vijana nchini Uganda ambao waliguswa na kutikiswa sana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, lakini wamegeuka na sasa wamefungua ukurasa mpya wa maisha, ni watu wema na wanaotegemewa na familia zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.