2015-02-15 13:54:28

Huduma ya huruma na mapendo!


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya Sita ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, inamwonesha jinsi ambavyo Yesu alivyokuwa anaguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya watu mbali mbali kiasi cha kujishikamanisha nao bila kuona kinyaa wala kuogopa Sheria ya Musa, kiasi hata cha kumgusa na kumponya mgonjwa mwenye ukoma, aliyekuwa ametengwa na jamii. RealAudioMP3

Yesu alitenda yote kwa huruma na mapendo, kiasi hata cha kuweza kuwarejesha tena katika Jamii wale waliokuwa wametengwa na kusukumizwa pembezoni kutokana na magonjwa na hali yao ya maisha!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 15 Februari 2015 wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, akiwa ameambatana na Makardinali wapya waliosimikwa siku ya Jumamosi, kwenye Liturujia ya Neno la Mungu. Wagonjwa wa ukoma walitengwa na jamii katika medani mbali mbali za maisha, kiasi kwamba walijisikia kuwa ni wadhambi kutokana na maradhi yaliyokuwa yanawaandama; hawa walikuwa ni sawa na maiti zilizokuwa zinatembea. Ni watu waliokumbana na adha mbali mbali za maisha, kiasi hata cha kutoweza kukutana na watu wengine ndani ya jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo la Sheria hii ya Musa lilikuwa ni kuwaokoa wazima na kuwalinda wenye haki, ili wasije wakakumbwa na maradhi ya ukoma, kwani ni heri kwa mtu mmoja kufariki dunia kuliko taifa zima kuangamia. Yesu Kristo analeta mabadiliko makubwa katika mtazamo wa Sheria hii, kwa kuipatia ukamilisho unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Ni mageuzi haya yaliyomwokoa pia yule mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, kwa kukazia: upendo, uhuru kamili na huruma ya Mungu inayookoa, ili wote waweze kukombolewa kwa kuufahamu ukweli. Yesu mwenyewe anaonesha kwamba, amekuja ili kuwaganga wanaoteseka, kuponya madonda yao na hatimaye, kuwarejesha tena katika Familia ya Mungu; jambo ambalo kwa wengi lilikuwa ni Kashfa ya Mwaka!

Lakini, Yesu hakuogopa, bali aliendelea kutenda, kwani hata leo hii kuna hatari inayoweza kujitokeza katika mantiki hii: kwanza kuna hatari ya kuogopa kuwapoteza wale waliokolewa na pili kutaka kuwaokoa wale waliopotea. Lakini anasema Baba Mtakatifu kwamba, mantiki ya Mungu inajikita katika huruma na mapendo yanayoshinda ubaya na hivyo kumkirimia mwanadamu wokovu.

Mantiki na mwelekeo huu ndio ambao Mama Kanisa katika historia ya maisha na utume wake ameendelea kuitekeleza kwa uaminifu, kwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, jambo lililoleta toba na wongofu wa ndani; watu wa Mataifa wakakumbatia Injili ya Kristo pasi ya kulazimika kushika Sheria za Musa. Watu wa Mataifa wakaingia na kuwa ni sehemu ya Kanisa; wakaguswa na kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao.

Huu ndio msimamo wa Mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu; mwelekeo uliooneshwa na Baba mwenye huruma, kwa kutokuhukumu, bali kuganga madonda na majeraha ya dhambi; ili kuwakumbusha kwamba, wagonjwa ndio wanaomhitaji tabibu, ili waweze tena kutubu na kukumbatia huruma na upendo wa Mungu. Kweli Yesu anaokoa na kumweka mtu huru hata na mawazo potofu. Huu ndio mwelekeo wa fadhila ya upendo ambao unajikita katika huruma, unathubutu na kushirikisha. Upendo wa kweli hauna masharti unatolewa bure na kwamba, lugha ya upendo inagusa na kuponya na hivyo kumchangamotisha aliyeponywa kutangaza matendo makuu ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawaambia Makardinali kwamba, hii ndiyo mantiki ya Yesu na njia ambayo Kanisa linafuata kwa kuwapokea na kuwaingiza tena katika Kanisa kwa moyo na ujasiri wa Kiinjili wale wote wanaobisha hodi katika malango ya Kanisa. Ni mwelekeo wa kujisadaka kwa ajili ya wengine, kielelezo makini cha dhamana na utume wa Ukardinali. Ni changamoto ya kujifunza kutoka kwa Bikira Maria aliyeteseka moyoni mwake na aliyelazimika kukimbilia Misri ili kumwokoa Mtoto Yesu, ili aweze kuwaombea viongozi wa Kanisa kuwa kweli ni watumishi waaminifu wa Mungu, kwa kuonesha huruma na mapendo bila ya kutaka kumezwa na mafaniko ya kidunia.

Baba Mtakatifu anawaalika Makardinali kuwatumikia na kuwaimarisha Watu wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, kwa kuwakumbatia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwa njia hii watakuwa wanamtukia Yesu Msulubiwa. Wajitahidi kumwona Yesu kati ya watu wanaoteseka na kuhangaika na maisha; waamini waliopoteza zawadi ya imani; watu waliokengeuka; wagonjwa na wasiokuwa na fursa za ajira; wanaotengwa na kubezwa. Mtakatifu Francisko wa Assisi awe ni mfano wa kuwakumbatia wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa njia hii, watu watawathamini na kuwaamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.