2015-02-14 14:41:08

Nguzo ya Upendo!


Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumamosi, tarehe 14 Februari 2015 amewatangaza Makardinali wapya 20 na kuwapatia kofia nyekundu alama ya ushuhuda wao, pete ya ukardinali pamoja na kuwapangia Makanisa ya huduma mjini Roma. Makardinali wapya wamekiri Kanuni ya Imani na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake. Ibada hii imehudhuriwa pia na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI.

Itakumbukwa kwamba, Kanisa Barani Afrika limebahatika kuwapata Makardinali wapya watatu nao ni: Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Addis Ababa, Ethiopia na Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Wa pili ni Kardinali Arlindo Gomes Furtado, Askofu wa Santiago de Cape Verde, kutoka katika Visiwa vya Cape Verde. Tatu ni Kardinali Julio Duarte Langa, Askofu mstaafu wa Jimbo la Xai-Xai, Msumbiji.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amewakumbusha Makardinali kwamba, hiki si cheo cha kujivunia, bali ni nguzo thabiti katika maisha na utume wa Kanisa; ni kielelezo cha upendo na umoja wa Kanisa kwani Kanisa la Roma linatekeleza wajibu msingi katika huduma ya upendo, inayopaswa kujionesha kwa njia ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakifuatia Makardinali. Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorinto sura ya 12: 31 hadi sura ya 13: 13 anafafanua sifa ya upendo isiyosikilizwa kwa umakini mkubwa na kumwilishwa na Bikira Maria.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Yesu Kristo ni upendo kamili uliomwilishwa, awasaidie kuweza kupokea Neno hili na kutembea katika njia hii, kwa kuwa wanyenyekevu na wapendelevu kama ilivyo kwa mama kwani upendo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayokuwa na kukomaa mahali palipo na unyenyekevu na upole. Upendo ni ukuu unaojionesha katika fadhila ya huduma ndani ya Kanisa mintarafu Moyo wa Kristo; sawa na Ukatoliki, unaomtaka mtu kupenda bila mipaka akizingatia uaminifu; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Upendo unawakumbatia wote: wakubwa kwa wadogo; kwa kuwatikia mema.

Baba Mtakatifu anasema, muujiza wa upendo ni kwamba: upendo hauhusudu; upendo hautakabari, haujivuni kwani ni tabia ya binadamu wa nyakati mbali mbali kujikuta anatambukia katika wivu na majivuno, kielelezo cha ubinadamu uliojeruhiwa kutokana na dhambi ya asili; hali ambayo inaweza kuwagusa hata viongozi wa Kanisa; lakini upendo wa Kimungu ndani mwao, ulete mabadiliko na kumwonesha Kristo anayeishi ndani mwao, kwani Yesu ni kielelezo cha upendo mkalimifu.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, upendo haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake, kwani upendo unaheshimu utu wa mtu; unatambua hali na mahitaji yake, lakini kwa mtu mwenye ubinafsi atajikuta anatafuta mafao yake binafsi badala ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo; kwa kuwaheshimu na kuwatakia mema wengine. Upendo hauhesabu mabaya na unamwokoa mtu kutoka katika hasira na chuki ya kutaka kulipiza kisasi; mambo ambayo kamwe hayawezi kuvumiliwa kwa kiongozi wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, upendo haufurahii udhalimu bali hufurahi pamoja na kweli, changamoto kwa viongozi wa Kanisa kujikita katika kutenda haki na kufurahia ukweli unaopata utimilifu wake katika mwili wa Yesu Kristo, chemchemi hai ya furaha kwa waja wake. Kiongozi wa Kanisa awe ni kielelezo cha haki na huduma ya furaha katika ukweli.

Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote; haya ni maneno makuu anasema Baba Mtakatifu yanayoweza kuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji, ili kuuwezesha upendo wa Kristo uliomiminwa mioyoni mwa waamini kwa njia ya Roho Mtakatifu kumwilishwa, ili kutoa msamaha, kuwa na imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kuendeleza mchakato wa kuwamegea wengine matumaini, ili kuvumilia hali mbali mbali za maisha, huku wakiwa wameungana na Yesu, aliyeshikamana na binadamu kwa njia ya upendo hata akajitwika dhambi zao zote.

Baba Mtakatifu anasema, Mungu ni upendo, changamoto kwa viongozi wa Kanisa kuwa wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, ili kweli waweze kuwa ni nguzo za unyenyekevu kwa dhamana na wajibu wanaokabidhiwa na Mama Kanisa kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu. Makardinali watambue kwamba, wao ni kielelezo cha upendo unaojionesha kwa njia ya unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu anayewamiminia upendo wa Mungu mioyoni mwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.