2015-02-14 11:50:33

Kimeeleweka: Uchaguzi mkuu ni 27 Novemba 2016


Tume Huru ya Uchaguzi nchini DRC imetangaza kwamba, uchaguzi mkuu nchini humo unatarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2016 na kwamba, matokeo ya awali ya uchaguzi huo yatatangazwa hapo tarehe 7 Desemba 2016 na matokeo ya jumla yatakuwa tayari katika kipindi cha siku kumi mara baada ya kuhitimisha uchaguzi mkuu. Huu utakuwa ni uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge, kadiri ya Katiba ya DRC.

Hayo yamebainishwa na Bwana Jean-Pierre Kalamba, Msemaji mkuu wa Tume huru ya uchaguzi nchini DRC. Taarifa inabainisha kwamba, uchaguzi wa Senate utafanyika mwezi Oktoba, 2015 na uchaguzi wa Serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika mwezi Januari 2016.

Hivi karibuni hali ya hewa kisiasa nchini DRC ilichafuka kiasi cha kusababisha maafa pamoja na uharibifu wa miundo mbinu, kwa kukataa mchakato wa kutaka kubadilisha Katiba ya Nchi ili kumruhusu Rais Joseph Kabila kuwania tena madaraka.







All the contents on this site are copyrighted ©.