Baraza la Makardinali katika mkutano wake wa siku mbili uliokuwa unafanyika mjini
Vatican, linampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ujasiri wake aliouonesha katika
kuanzisha mchakato wa mageuzi ndani ya Sekretarieti ya Vatican, kwani hali ya uchumi
ilikuwa imefikia pabaya.
Kanisa halina
budi kuendelea kujikita katika misingi ya ukweli, uwazi, uadilifu na maadili katika
matumizi ya fedha na mali ya Kanisa ambayo kimsingi ni kwa ajili ya mchakato wa Uinjilishaji
wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Huu ni muhtasari
ambao umetolewa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican wakati akizungumza
na waandishi wa habari mjini Vatican siku ya Ijumaa na kusema kwamba, Makardinali
164 wameshiriki katika mkutano wao uliokuwa unaongozwa na Baba Mtakatifu Francisko,
ili kuchangia mchakato wa mageuzi unaoendelea kuvaliwa njuga na Kanisa kwa wakati
huu, ili kuliwezesha Kanisa, kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara.
Makardinali
wamejadili kwa kina na mapana kuhusu mada na taasisi mbali mbali za uchumi zinazosimamiwa
na Vatican, chini ya uongozi wa Kardinali George Pell na Kardinali Reinhard Marx.
Makardinali wamechangia mawazo kuhusu Benki kuu ya Vatican, IOR na matarajio yake
kwa siku za usoni. Kimsingi Makardinali wameridhika na hatua mbali mbali ambazo zimechukuliwa
kama sehemu ya mchakato wa mabadiliko katika sekta ya uchumi mjini Vatican.
Makardinali
wanasema, kanuni ya ukweli, uwazi, uadilifu, weledi na maadili ni mambo msingi sana
katika mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya Kanisa. Mabadiliko yanayoendelea
kufanyika mjini Vatican, hayana budi kuendelezwa na kutekelezwa hata katika Makanisa
mahalia na taasisi zote zinazosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa. Hizi ndizo cheche
za mabadiliko zinazoletwa na Baba Mtakatifu Francisko, wanasema Makardinali, "hapa
hakuna kulala hadi kieleweke"!
Makardinali wameendesha mkutano wao anasema
Padre Federico Lombardi katika hali ya amani, utulivu, udugu na mshikamano, kwa kupembua
kwa kina na mapana mahusiano kati ya Sekretarieti kuu ya Vatican, Makanisa mahalia
pamoja na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki. Hapa Makardinali wamekazia kanuni ya auni
inayoonesha huduma ya upendo inayotolewa na Sekretarieti ya Vatican kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya Kanisa mahalia pamoja na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki.
Makardinali
wameonesha dhamana, wajibu na utume unaopaswa kutekelezwa na Sekretarieti kuu ya Vatican,
kwa kusoma alama za nyakati pamoja na kuyasaidia Makanisa yale ambayo bado "yanachechemea"
katika masuala mbali mbali, ili kuweza kutekeleza utume wake barabara. Muundo wa utekelezaji
wa kazi za Sekretarieti kuu ya Vatican hauna budi wanasema Makardinali kujikita katika
uratibu mzuri unaofumbatwa katika mshikamano wa Kikanisa na kanuni ya auni badala
ya mtindo wa kuzungumza na kufanya vikao ambavyo wakati mwingine havina tija wala
mashiko kwa ustawi na maendeleo ya Kanisa.
Makardinali wamesisitiza kwamba,
msimamo wa Kanisa katika masuala mbali mbali na ushirikiano wa kimataifa hauna budi
kuwa wazi na endelevu, kwa kuhakikisha kwamba, Mabaraza na taasisi za Kipapa zinazohusika
na masuala haya zinashirikishwa kikamilifu, ili kuwa na kauli na msimamo mmoja; hali
ambayo inahitaji kuratibiwa kikamilifu.
Makardinali wanasema kwamba, mchakato
wa mageuzi unapania pia kupunguza idadi ya wafanyakazi, kwa kuzingatia sifa na vigezo
vinavyotakiwa na kwamba, Sekretarieti ya Vatican haina budi kuonesha ile taswira ya
Kanisa la Kiulimwengu kwa kuwa na wafanyakazi kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Nafasi ya walei, hasa wanawake ndani ya Kanisa imesisitiziwa sana na Makardinali na
kwamba, mageuzi haya ni mchakato endelevu mintarafu Mafundisho ya Kanisa.
Mwishoni
Makardinali wameridhia kwamba, utekelezaji wa maamuzi ambayo tayari yamekwishafikiwa
unaweza kuanza taratibu, badala ya kuendelea kukaa na kusubiri kukamilisha mfumo mzima
wa mageuzi, ambao kimsingi utahitaji muda mrefu zaidi.
Na Padre Richard A.
Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.