Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, Baraza la Maaskofu Katoliki Australia
kwa namna ya pekee kabisa, linawaalika Watawa mbali mbali nchini humo, kuhakikisha
kwamba, wanaishirikisha Familia ya Mungu nchini Australia upendo na tabasamu kutoka
kwa Mwenyezi Mungu. Maadhimisho haya
yanakwenda sanjari na Jubilee ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa
Vatican walipotangaza Waraka wa Upendo Mkamilifu, Perfectae caritatis, ili watawa
waweze kupyaisha maisha yao ndani ya Kanisa, tayari kutoka kifua mbele kuwatangazia
Watu wa Mataifa, Injili ya Furaha na Matumaini kwa wale waliokata tamaa. Hii ni
changamoto kwa watawa kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko
kutokana na maisha na utume wao unaomwilishwa katika huduma makini kwa Familia ya
Mungu inayowazunguka. Watawa waendelee kuwa ni sauti ya kinabii inayowaamsha walimwengu,
daima, wakiwa ni watu wenye furaha, kwa kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa
na Mwenyezi Mungu. Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linaendelea kuwahimiza
watawa kuhakikisha kwamba, wanasimika maisha yao katika sala na tafakari ya Neno la
Mungu, ili waweze kujifunza kutoka kwa Yesu Kristo, ambaye ni Mwalimu na Bwana. Hata
pale wanapokuwa wanatekeleza wajibu na dhamana yao, watawa waoneshe umuhimu wa sala
na tafakari ya Neno la Mungu. Walimwengu wanapenda kuwaona watawa wakishuhudia
kwa njia ya maisha yao, huruma na upendo wa Mungu, unaoleta mvuto kwa watu kutaka
kuchuchumilia yaliyo: kweli, mema na matakatifu. Watawa wawe ni cheche za matumaini
kwa wale waliokata tamaa ya maisha; wawe tayari kujisadaka pale wanaohitajika kutoa
huduma kwa watu; watawa wawe ni faraja kwa wale waliopondeka moyo; wawe tayari kuwaonjesha
waamini wanaokimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili hatimaye,
waweze kuonja furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kimsingi,
watawa wote wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawaonjesha wengine
furaha, upendo na huruma ya Mungu. Watambue mapungufu yao ya kibinadamu na waendelee
kujitakatifuza, ili kujenga na kudumisha umoja unaojionesha katika maisha ya kijumuiya,
ili kuwaamsha walimwengu wanaojikita katika ubinafsi na migawanyiko. Watawa wawe ni
chachu inayokoleza maisha ya watu ili kutafuta mafao ya wengi. Baraza la Maaskofu
Katoliki Australia linawaalika Watawa katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani,
kuhakikisha kwamba, kweli wanaendelea kuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini. Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.