Jumuiya ya Kimataifa inatarajiwa kufanya mkutano mkuu hapo tarehe 3 Machi 2015, huko
Brusseles, Ubelgiji ili kupembua kwa kina na mapana hali halisi ya ugonjwa wa Ebola
na mapambano yake pamoja na kuibua mbinu mkakati utakaotokomeza kabisa ugonjwa wa
Ebola ambao umekuwa ni tishio kwa maisha ya wananchi wengi duniani, lakini kwa namna
ya pekee katika Nchi za Afrika Magharibi.
Mkutano huu utaratibiwa na viongozi
wakuu wa nchi kutoka Guinea, Sierra Leone, Liberia, Togo, Umoja wa Mataifa pamoja
na Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS. Kutakuwepo na wajumbe 80
kutoka Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya pamoja na Mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo
yanajikita katika mapambano dhidi ya janga la Ebola duniani, bila kuisahau Benki ya
Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa. Taarifa zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna
zaidi ya wagonjwa 22, 000 walioambukizwa Virusi vya Ebola na kati yao wagonjwa 8.
800 wamekwisha fariki dunia.