2015-02-13 09:06:49

Kanuni za mabadiliko!


Baba Mtakatifu Francisko tangu alipokabidhiwa dhamana na utume wa kuliongoza Kanisa Katoliki, alishauriwa na Makardinali kufanya mageuzi makubwa katika Sekretarieti ya Vatican ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kikanisa kwa kusoma alama za nyakati. Tangu mwaka 2013 Baba Mtakatifu anajielekeza zaidi katika masuala makuu matatu katika mageuzi haya: maboresho, udogo na ubora; mambo ambayo ni mwongozo wa Baraza la Makardinali ambalo linaendelea kufanya kazi bega kwa bega na Baba Mtakatifu Francisko.

Mkutano wa Makardinali uliofunguliwa Alhamisi, 12 Februari 2015 na Baba Mtakatifu unapania kutoa ushauri aminifu na endelevu utakaomwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kuliongoza Kanisa la Kristo; kwa kuzingatia ubora, ufanisi na tija, kama alivyobainisha Askofu Marcello Semeraro, Katibu wa Baraza la Makardinali, wakati akiwasilisha taarifa elekezi kwa Makardinali. Hii ni taarifa iliyotolewa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, siku ya Alhamisi.

Kwa upande wake anasema Padre Lombardi, Kardinali Rodriguez Maradiaga amefafanua kwa kina na mapana: kanuni, dira na mwongozo wa mageuzi ambayo Baba Mtakatifu anapania kufanya kwenye Sekretarieti ya Vatican. Amebainisha asili na uwezekano wa kuunganisha baadhi ya Mabaraza ya Kipapa, ili kupunguza ukubwa wa Sekretarieti, kwa kujikita katika ubora, tija na ufanisi. Sekretarieti kuu ya mji wa Vatican inawajibu wa kuratibu shughuli mbali mbali zinazofanywa na Mabaraza ya Kipapa, kumbe hapa hakuna wazo la kuanzisha tena miundo mipya.

Padre Lombardi anabainisha kwamba, ufafanuzi wa kitaalimungu na kisheria uliotolewa unaonesha kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kuunganisha mabaraza makuu mawili ambayo yanamwingiliano wa tema pamoja na utendaji wake wa kazi: "Familia, Walei na Maisha" na upande wa pili ni "Upendo, haki na amani.

Hapa baadhi ya Mabaraza ya Kipapa pamoja na taasisi mbali mbali zinaweza kuunganishwa katika makundi haya mawili na hivyo kuunda Mabaraza makuu mawili, yaani: Baraza la Kipapa la Familia, Walei na Maisha; pili ni Baraza la Kipapa la Upendo, haki na amani.

Padre Lombardi anasema, muundo wa Kisinodi ni kati ya mambo ambayo yanapatiwa kipaumbele cha pekee katika utekelezaji mpya wa shughuli na mikakati ya Sekretarieti kuu; changamoto ni kuweza kuteuwa watu watakaotekeleza dhamana hii, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma na uwajibikaji. Makardinali wanakumbushwa kwamba, mabadiliko haya ni makubwa pengine yatachukua muda mrefu zaidi kabla ya kuanza utekelezaji wake. Hapa kuna haja ya kuunda Tume maalum itakayoshughulikia mwongozo wa uundaji wa Mabaraza haya na hatimaye, kufanyiwa tathmini na Baraza la Makardinali katika vikao vyake na baadaye kutolewa maoni na Makardinali, Maaskofu na Mabaraza ya Kipapa.

Tume ya Makardinali itakuwa na dhamana ya kuandaa muswada ambao utawasilishwa kwa Baba Mtakatifu kwa ajili ya kufanyiwa maamuzi na hatimaye, utekelezaji wake na kwamba, baadhi ya mambo yanaweza kuanza kutekelezwa kwa majaribio wakati ambapo Kanisa linaendelea kusubiri Waraka kamili unaobainisha mageuzi haya ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.