Mapambano dhidi ya Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria pamoja na sakata
la vikatuni vya kashfa dhidi ya dini ya Kiislam, ni mambo ambayo yanachangia uwepo
wa hali tete ya mahusiano kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo nchini Niger.
Hali hii ilipelekea hivi karibuni, Makanisa kadhaa kuchomwa moto kwa kisingizio cha
misimamo mikali ya kidini.
Uamuzi uliofanywa na Serikali ya Niger ya kuunga
mkono mapambano dhidi ya Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram kutoka Nigeria yametibua
tena nyongo za waamini wa dini ya Kiislam nchini Niger kwa kisingizio kwamba, haya
ni mashambulizi dhidi ya Kikundi kinachotetea misingi ya dini ya Kiislam, jambo ambalo
si kweli kabisa!
Kwa sasa Nchi za Afrika Magharibi, yaani: Nigeria, Cameroon,
Chad na Benin, zimeamua kuunganisha nguvu zao dhidi ya Kikundi cha kigaidi cha Boko
Haram na cheche za matumaini zinaanza kuonekana, ingawa Boko Haram kinaendelea kusababisha
maafa makubwa zaidi kwa watu na mali zao. Vijana wengi wanaajiriwa kwenye makundi
ya kigaidi kutokana na ukosefu wa ajira, unaowasababishia ukata mkubwa pamoja na kukosa
dira na mwelekeo wa maisha.
Mashuhuda wanasema, ni vijana hawa ndio waliohusika
katika matukio ya kuchomwa moto kwa makanisa nchini Niger hivi karibuni. Itakumbukwa
kwamba, tukio kama hili la vijana wenye misimamo mikali ya kidini, liliwahi kutokea
kunako mwaka 2012. Matukio yote haya ni cheche dhidi ya Wakristo huko Niger, jambo
ambalo ni tishio kwa usalama na maisha ya watu; uhuru wa kuabudu; utu na heshima ya
binadamu.
Kanisa linapenda kujielekeza zaidi katika majadiliano yanayojikita
katika uhalisia wa maisha kwa kusaidiana, kuheshimiana na kupendana kama watu wa jamii
moja, ili kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa na kwamba, dini kisiwe ni chanzo
cha vurugu, kinzani na misigano ya kijamii, kwani wanaoumia ni wanyonge ndani ya jamii.
Wanasiasa wakati mwingine wamekuwa ni chachu ya vurugu za kidini kwa ajili ya masilahi
binafsi, jambo ambalo ni hatari kabisa kwa mfungamano na mshikamano wa kitaifa.