2015-02-12 07:41:25

Zaidi ya watu 232 wamekufa maji!


Bado wahamiaji wanaendelea kupoteza maisha yao katika Bahari ya Mediterrania hata baada ya kunyanyaswa na kudhulumiwa na wafanyabiashara haramu ya binadamu. Taarifa kutoka Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, wahamiaji 232 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, wamekufa maji na kwamba, kuna mashua moja imepotea ambayo pia inasadikiwa kuwa na idadi kubwa ya wahamiaji, ambao pia wanahofiwa kwamba, wamefariki dunia.

Ikiwa kama takwimu za awali na ambazo zimekwisha kutolewa hadi sasa zitaweza kuthibitishwa, basi kuna wahamiaji zaidi ya 400 watakuwa wamekufa maji katika siku za hivi karibuni. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 11 Februari wakati wa Katekesi yake, amesema kwamba, anaendelea kufuatilia taarifa za maafa yanayoendelea kujitokeza kwenye Bahari ya Mediterrania kwa masikitiko makubwa, kwani kuna watu bado wanaendelea kupoteza maisha yao na kwamba, anapenda kuwahakikishia wote sala na uwepo wake kiroho!

Mashuhuda wanasema kwamba, hali ya hewa ilikuwa mbaya, lakini wafanyabiashara haramu wa binadamu wakawalazimisha kupanda kwenye mashua na kuanza safari, vinginevyo, wangekiona cha mtema kuni. Mashua nne zilizokuwa zimebeba wahamiaji 460, wakati wakiwa njiani, mashua moja ikazama maji na abiria wote wakapoteza maisha.

Hii ni safari iliyoanza huko Tripoli, Libya, Mwishoni mwa Juma. Baadhi ya wahamiaji waliweza kuokolewa na Kikosi cha Wanamaji wa Italia, lakini wengi wao walikuwa na hali mbaya sana kiasi cha kuhitaji huduma ya haraka. Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kujadili kuhusu hatima ya wahamiaji kwenye Bahari ya Meditterania, lakini watu wanaendelea kupoteza maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.