2015-02-12 11:40:16

Mambo ya kuzingatia!


Kardinali Joao Braz de Avis, Rais wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, katika maadhimisho ya Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio amezindua rasmi Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa ulioitishwa na Baba Mtakatifu Francisko, mwaka unaotarajiwa kutoa nafasi kwa watawa kufanya tafakari ya kina ili kuangalia hija ya maisha na utume wao katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, tangu kuadhimishwa kwa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. RealAudioMP3

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko na kufanyiwa kazi na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, ili kwa pamoja kuweza kutafakari changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusiana na maisha ya kitawa katika Waraka wake wa “Perfectae caritatis” Mapendo Kamili.

Lengo ni kutoa nafasi ya kwanza kwa maisha ya kiroho, maisha ya kijumuiya, mashauri ya kiinjili; malezi na majiundo endelevu; uanzishaji wa Mashirika mapya na changamoto zake; kupungua kwa idadi ya miito na athari zake pamoja kuangalia mshikamano wa viongozi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, wanavyoweza kushirikiana katika mchakato wa Uinjilishaji mpya katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Kardinali De Avis anasema katika maadhimisho ya mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wamepembua kwa kina na mapana jinsi ya kuweka “divai mpya katika viriba vipya” kwa kutafakari matendo ya Mungu yaliyojitokeza katika kipindi cha miaka 50 iliyopita: Jambo la kwanza wameangalia majiundo awali na endelevu kwa watawa; maisha ya kijumuiya na changamoto zake; uongozi wa watawa na magumu yake katika ulimwengu wa utandawazi pamoja na matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii.

Sehemu zote hizi zimeonesha maboresho makubwa lakini yenye kubeba dhamana na changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Baraza la Kipapa linaendea kuandaa Waraka utakaosaidia kukabiliana na changamoto hizi kwa imani na matumaini makubwa, kwa kujiachilia zaidi mikononi mwa Mwenyezi Mungu, bila ya kukata wala kukatishwa tamaa. Mwenyezi Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake, bila shaka atawasaidia watawa kuanza tena hija ya maisha yao wakiwa na matumaini na furaha tele hata pale wanapokutana na Misalaba ya maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anaonesha mapendo makubwa kwa watawa katika maisha na utume wa Kanisa; ni kiongozi anayejitambua kuwa ni mtawa, jambo ambalo linawapatia watawa furaha kubwa anasema Kardinali Joao Braz de Aviz. Baba Mtakatifu anakazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa sala, maisha ya kijumuiya kama wafuasi amini wa Yesu Kristo; kwa kuendelea kumwilisha karama za waanzilishi wa Mashirika yao kwani hii ni zawadi kubwa kwa Kanisa, inayopaswa kutekelezwa kwa kusoma alama za nyakati. Watawa kwa mara nyingine tena wanatumwa kwenda ulimwenguni kujadiliana na kusaidia kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wao kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.