Baraza la Makardinali Washauri kuhusu mabadiliko ya Sekretarieti ya limehitimisha
kikao chake cha tisa kwa ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Makardinali hawa watakutana
tena kuanzia tarehe 13 hadi 15 Aprili 2015. Hayo yamebainishwa na Padre Federico Lombardi,
Msemaji mkuu wa Vatican wakati akizungumza na waandishi wa Habari mjini Vatican siku
ya Jumatano, tarehe 11 Februari 2015.
Kwa sasa kuna Waraka ambao unaendelea
kuandaliwa ambao kimsingi unahitaji muda mrefu, kwani hii itakuwa ni Katiba mpya na
wala si tu marekebisho ya nyaraka zilizokwishawahi kutolewa kuhusu Sekretarieti ya
Vatican. Kikao cha mwisho kimeandaa taarifa kwa ajili ya kikao cha Makardinali wote
ambacho kinaanza, Alhamisi, tarehe 12 Februari 2015 na utangulizi wake unatolewa na
Kardinali Rodriguez Maradiaga.
Baraza la Makardinali limefafanuliwa kuhusu:
kazi, majukumu na maendeleo yaliyokwishafikiwa na Sekretarieti pamoja na Baraza la
Kipapa la Uchumi. Wamesikiliza pia taarifa ya Tume ya Kipapa ya kulinda watoto wadogo
dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Alhamisi, Makardinali wote wanafanya kikao ambacho
kinatanguliwa na taarifa elekezi kutoka kwa Baraza la Makardinali na baadaye Makardinali
wataanza kuchangia maoni yao.