Tazama inavyopendeza ndugu kukaa kwa pamoja katika umoja na mapendo, lakini kwa namna
ya pekee wakati huu, Kanisa linapowakaribisha Makardinali wateule 20, kwa pamoja kuweza
kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Kikanisa. Ni maneno ya Baba Mtakatifu
Francisko kwa Makardinali walioanza mkutano wao wa kawaida mjini Vatican, Alhamisi,
tarehe 12 Februari 2015.
Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wote wa Kanisa
walioandaa tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa, kama sehemu ya mchakato
wa maandalizi ya muswada wa Waraka unaopania kufanya mageuzi makubwa katika Sekretarieti
ya Vatican. Huu ni muhtasari wa mchango wa mawazo kutoka kutoka kwa wakuu wa Mabaraza
ya Kipapa na wataalam katika sekta husika, lengo ni kuleta maboresho ya kazi zinazotekelezwa
na Sekretarieti ya Vatican, ili kuongeza tija na ufanisi; ukweli na uwazi; mambo msingi
yanayojenga na kuimarisha mwono wa kisinodi na mshikamano wa kikanisa.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, lengo la mabadiliko yanayofanyiwa kazi kwa sasa ni kuliwezesha
Kanisa kuwa shuhuda makini, ili kusaidia mchakato wa maboresho katika azma ya Uinjilishaji;
kukuza na kuimarisha majadiliano ya kiekumene na kidini; changamoto iliyotolewa na
Makardinali katika mikutano yao elekezi. Sekretarieti ya Vatican inapaswa kuboreshwa
zaidi, ili kutoa utambulisho wenye mvuto na maguso pamoja na kuendelea kumsaidia Khalifa
wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Lengo kuu ni kuimarisha
umoja katika imani, upendo na mshikamano kati ya watu wa Mungu na kuendeleza utume
wa Kanisa ulimwenguni.
Baba Mtakatifu anakiri kwamba, hapa kuna kazi pevu,
ili kuweza kufikia lengo, kwani kunahitajika muda, ari, lakini zaidi ushirikiano na
wadau mbali mbali sanjari na kuendelea kumwomba Roho Mtakatifu, aliongoze Kanisa,
katika maamuzi na mang'amuzi yake. Mkutano huu utaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa
anasema Baba Mtakatifu, ikiwa kama kila Kardinali atachangia mawazo pamoja na kuendelea
kuwa waaminifu kwa Mafundisho ya Kanisa, kwa ajili ya amani na ustawi wa roho za waamini.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.