Tukio la Makardinali kukusanyika kumzunguka Khalifa wa Mtakatifu Petro, chini ya usimamizi
na uongozi wa Roho Mtakatifu, ni kielelezo cha imani na utashi wa kutaka kushirikiana
na Baba Mtakatifu kwa karibu zaidi, ili kumwezesha kutekeleza dhamana na utume wake
kwa uaminifu na tija zaidi.
Makardinali wa Kanisa Katoliki wanayo nafasi muhimu
sana katika maisha na utume wa Kanisa, kwani wao ni washauri wakuu kwa Khalifa wa
Mtakatifu Petro katika utekelezaji wa dhamana yake kama kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki.
Hizi ni salam na matashi mema yaliyotolewa na Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali
wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Makardinali mjini Vatican, siku ya Alhamisi, tarehe
12 Februari 2015 na kukazia kwamba, Makardinali kutoka sehemu mbali mbali za dunia,
wanapenda kushirikisha mawazo, uzoefu na manga'muzi yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya Kanisa la Kristo.
Kardinali Sodano anasema kuna jumla ya Makardinali 228,
lakini hawakuweza kuhudhuria wote kutokana na umri, ugonjwa na bila kumsahau Kardinali
Karl Joseph Becker, SJ, aliyefariki dunia hivi karibuni na anatarajiwa kusindikizwa
katika usingizi wa milele katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Kardinali
Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, Jumatatu, tarehe 16 Februari 2015, majira ya
saa 8. 45 mchana kwa Saa za Ulaya. Baba Mtakatifu atahitimisha sala kwa Ibada ya Maziko.
Ibada hii itafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.
Kardinali
Sodano anasema, wanapenda kuchangia mchakato wa mageuzi makubwa yanayotarajiwa kufanywa
na Mama Kanisa katika Katiba ya Kitume, Mchungaji Mwema, "Pastor Bonus", matunda ya
marekebisho ya Nyaraka mbali mbali zilizotungwa na Papa Pio wa Kumi, Mwenyeheri Paulo
VI na Mtakatifu Yohane Paulo II, walioleta muundo wa Sekretarieti ya Vatican kama
ulivyo kwa sasa. Lengo ni kusoma alama za nyakati, ili kulisaidia Kanisa kukabiliana
na changamoto katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo na kwa ajili ya sifa
na utukufu wa Mungu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.